Update:

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MDOGO WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBUTUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu katika Majimbo ya Ukonga, Korogwe Vijijini, Monduli na kwenye Kata 23 za Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na Kanuni wakati wa uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa), Semistocles Kaijage ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi Uchaguzi huo mdogo jijini Dodoma.
Jaji Kaijage amewataka Wasimamizi hao kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili wapunguze na kuondoa malalamiko yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.
Amesema Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.
“ Tunakutana hapa kwa muda wa siku tatu (3) ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi,” Amesema Jaji Kaijage.
Aidha, amewataka Wasimamizi hoa waepuke madhara yanayotokana na ukiukaji wa Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi na akisisitiza kwamba katika kipindi hiki chaguzi zinafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya Kisiasa, kutoaminiana na wakati mwingine hutawaliwa na mihemko ambayo imekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Jaji Kaijage amewaeleza Wasimamizi hao kwamba wameaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo za usimamizi wa Uchaguzi kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo wajiamini na kujitambua.