Update:

TRA: WAFANYABIASHARA MSISUBIRI TAREHE ZA MWISHO KUOMBA MSAMAHA WA RIBA NA ADHABU YA KODI


WAFANYABIASHARA wenye malimbikizo ya madeni ya kodi wametakiwa kutuma maombi ya msamaha maalumu wa riba na adhabu kwenye malimbikizo hayo mapema kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018 ili waweze kunufaika na msamaha huo ambao umetolewa kwa lengo la kutoa unafuu kwa kuwapa fursa ya kulipa kodi ya msingi ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19.Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka wakati wa semina elekezi kwa wafanyabiashara, wadau na washauri wa wafanyabiashara kuhusu msamaha huo iliyofanyika leo mkoani Tabora.


"Nachukua fursa hii kutoa wito kwenu wafanyabiashara kutuma maombi ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi ambapo mwisho wa kutuma maombi ya msamaha huu ni tarehe 30 Novemba, 2018," alisema Mahendeka.


Mahendeka aliongeza kuwa "Mara nyingi wafanyabiashara huwa mnajitokeza mwishoni kabisa mwa tarehe zinazoonyesha mwisho wa kulipa, kuwasilisha au kutuma maombi fulani suala linalosababisha foleni na msongamano mkubwa katika kutoa huduma katika ofisi zetu. Nachukua fursa hii kuwaomba msisubiri tarehe za mwisho kuleta barua za maombi ya msamaha huu wa riba na adhabu ya madeni ya kodi na naomba mjue kwamba, huu ndio muda muafaka wa kila mwenye malimbikizo ya madeni kutuma maombi Ofisi ya TRA katika mkoa wake kikodi."

Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka akitoa elimu juu ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi wakati wa semina elekezi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali (hawapo pichani) iliyofanyika mkoani Tabora kwa lengo la kuwahamasisha wafanyabiashara hao kutuma maombi ya msamaha huo kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018.