Update:

Mwalimu ashikiliwa akidaiwa kuua mwanafunzi

Polisi mkoani Kagera inamshikilia mwalimu Respicius Patrick wa shule ya msingi Kibeta akituhumiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi wa darasa la tano, Siperius Eradius.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi alisema kifo cha mwanafunzi huyo kilitokea jana akipelekwa hospitali.

Alisema Patrick (50), ambaye ni mwalimu wa nidhamu anadaiwa kumpiga mwanafunzi huyo akihusishwa na upotevu wa mkoba wa mwalimu Herieth Gerard (46) uliokuwa na Sh75,000 na vitambulisho vyake. Baba wa mwanafunzi huyo, Justus Balilemwa alisema alimchukua mtoto huyo kituo cha watoto yatima cha Ntoma baada ya mama yake kufariki dunia akijifungua.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa Mkoa wa Kagera, Dk John Mwombeki alisema uchunguzi wa awali wa mwili wa mwanafunzi huyo unaonyesha alama zinazohusishwa na kupigwa.

Wakati huohuo, mwanafunzi wa kidato cha tano amelazwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi) akiuguza majeraha akidai kushambuliwa na wenzake.

Salim Mushumbusi (20) anayesoma mchepuo wa PCB katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Kwiro alishambuliwa Agosti 6. Mwanafunzi huyo aliyeripoti shuleni Julai 27 akizungumza na Mwananchi akiwa wodini alisema siku ya tukio akiwa anaota moto na wenzake, mmoja alisema skauti wana nguvu kuliko walimu, jambo lililomlazimu kuhoji.

Salim aliyemaliza kidato cha nne katika Shule ya St Joseph, Morogoro alisema kutokana na yeye kuhoji, skauti huyo alikasirika hivyo akiwa na wenzake wapatao 13 walimshambulia wakiwa wamemfungia chumbani.

Alisema baada ya walimu kufika alipelekwa Hospitali ya St. Francis Ifakara alikopatiwa matibabu kwa siku mbili na kuhamishiwa Moi.

Mkuu wa shule hiyo, Andrea Lazima hakupatikana kuzungumzia tukio hilo lakini makamu wake, John Kashamba alikiri kuwa Salim ni mwanafunzi wa shule hiyo na kumtaka mwandishi kuzungumza na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mahenge ambaye hakupatikana.

Faith Mushumbusi, ambaye ni mama wa Salim alisema amepokea Sh300,000 kutoka kwa uongozi wa shule kwa ajili ya matibabu ambazo hazitoshi kwa kuwa mwanaye hana bima ya afya.

Daktari wa Moi, Lemeri Mchome alisema Salim anasumbuliwa na maumivu mgongoni na hawezi kutumia miguu yake ambayo imekosa nguvu na analalamika kuwa na maumivu. Alisema wanatarajia kuendelea na vipimo kuangalia uti wa mgongo kubaini tatizo