Update:

MAHAKAMA YAKUBALI OMBI LA UPANDE WA JAMUHURI KESI YA VIGOGO CHADEMA IENDELEE

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubaliana na ombi la upande wa Jamuhuri la kutaka kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali na uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe iendelee na kupanga kusoma usikilizwaji wa awali (PH)
Julai 31 mwaka 2018.


Pia Mahakama imeruhusu upande wa mashtaka kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo mara moja baada ya PH kusomwa. Hayo yamefikiwa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri baada ya kesi hiyo kuja kwa kutajwa kutokana na kusimama kupisha maamuzi ya mahakama kuu.


Kutokana na maombi ya upande wa mashtaka yaliyokuwa yakiomba mahakama kuu kufanyia marejeo mwenendo wa kesi yao juu ya uamuzi wa mahakama ya Kisutu.Hata hivyo, Julai 20 mwaka 2018 Mahakama Kuu ilitoa uamuzi na kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa yalikuwa ni batili na kwamba yalikosa vigezo kisheria.


Mapema Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliomba Mahakama kulipangia shauri hilo tarehe ya kuwasomea washtakiwa PH kwa kuwa uamuzi wa mahakama kuu ulishatoka na ombi la utetezi kutupiliwa mbali. "Mheshimiwa, shauri hili leo limekuja kwa kutajwa kwa sababu tulikuwa tunasubiri maamuzi ya Mahakama Kuu, lakini kwa kuwa maamuzi yameishatolewa.


"Tunaomba tarehe ya kuja kuwasomea washtakiwa PH na kuanza kusikilizwa siku hiyo hiyo mfululizo kwa tarehe zitakazopangwa na mahakama," ameeleza Nchimbi,Hata hivyo, Wakili wa utetezi Nashon Nkungu kwa niaba Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya wanaowatetea washtakiwa amedai kuwa baada ya uamuzi ule wa Mahakama Kuu, washtakiwa wamefaili kusudio la kukata rufaa mahakama ya Rufani ambayo ilipokelewa Julai 20 mwaka 2018


" Kutokana na kusudio hilo la Rufaa tunaomba muda wa kutosha kabla ya kusomwa kwa PH kwa kuzingatia kuwa kuna rufaa," amedai Nkungu.Akijibu hoja hiyo, Wakili Nchimbi amedai mahakama inatakiwa kutoa maamuzi kwa kuzingatia mambo ambayo yako kwenye kumbu kumbu za mahakama, lakini mpaka sasa hakuna chochote kilichopo mbele ya mahakama kuhusu kusudio la kukata rufaa.


Baada ya mabishano ya pande zote mbili mahakama imekubaliana na ombi la Jamuhuri na kupanga kuhusu shauri kupangwa kwa PH na kuanza kusikilizwa.Pia imeruhusu upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao juu ya maombi yao ni yapi, je ni ya kutaka shauri lao liahirishwe kwa muda mrefu au lisimame kupisha rufaa?Mbali na Mbowe, washitakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.


Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime mjini, Matiko.Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 12, ambapo wanadaiwa kuwa walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu katika maeneo ya Viwanja vya Buibui, Mwananyamala na barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni.


Wanadaiwa kuwa Februari 16 mwaka huu katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washitakiwa hao wakiwa na wenzao 13 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani.

Baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

No comments