Update:

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage Atakiwa kutoa maelezo ya Serikali bungeni kuhusu mafuta leo saa 11 jioni

Spika wa Bunge, Job Ndugai ameishukia Serikali kuhusu madai ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kula akimtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kufikia leo Jumanne Mei 8, 2018 saa 11 jioni kuwasilisha bungeni taarifa ya kinachoendelea kuhusu jambo hilo ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi.
Ndugai ametoa kauli hiyo leo asubuhi bungeni mjini Dodoma wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe aliyehoji kuhusu bei ya mafuta, akidai imepanda na kujibiwa na Mwijage kuwa jambo hilo linashughulikiwa kwa maelezo kuwa kwa sasa umeibuka mvutano.
Tishio la kuadimika kwa mafuta ya kula linatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzizuia meli mbili zenye tani 62,000 za mafuta ya kula katika Bandari ya Dar es Salaam tangu mwezi uliopita
Utata wa kulipa kodi inayodaiwa na TRA, unatokana na madai ya mamlaka hiyo inayosema mafuta yaliyoingizwa ni safi ilhali wamiliki wakieleza ni ghafi.
Leo katika majibu yake, Mwijage baada ya kutoa maelezo marefu amesema alitoa ushauri kwa TRA kwamba wenye mafuta, “nusu ya mzigo ushushwe, tatizo linalokuja tunahukumiwa na historia, nashauri hii kazi unipe mimi, nitakuja saa 11 kukueleza kipi kimetokea.” Baada ya kauli hiyo ya Mwijage, Spika Ndugai alisimama na kusema: “Nalikubali hili la saa 11 na bahati nzuri nitakuwa hapa. Tunapokuwa bungeni lazima tuseme ukweli yaani iko hivyo.
Tukiligeuza Bunge hili kuwa mahali pa kubangazia hivi, mimi niombe saa 11 tupate majibu ya uhakika.”

No comments