Update:

Nkamia atangaza rasmi kuutaka urais wa Simba

ALIYEKUWA Katibu Mwenezi wa Simba, ambaye ni Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, ametangaza nia yake ya kutaka kugombea nafasi ya urais wa klabu hiyo katika uchaguzi mkuu ujao, ambao unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Juma Nkamia.
Nkamia alitangaza nia yake hiyo juzi, ikiwa ni baada ya tamko la mfanyabiashara, Mohamed Dewji 'Mo' kuweka wazi kwamba ameridhia kuwekeza katika klabu hiyo kwa kiasi cha asilimia 49 huku asilimia 51 ikibaki kwa wanachama kama mwongozo wa serikali ulivyoelekeza.
"Natarajia kugombea ili kuiongoza Simba, naomba uniunge mkono (jina tunalihifadhi) muda ukifika," alisema kwa kifupi Nkamia na kuanzisha mjadala wa nani anasifa ya kugombea katika uchaguzi ujao wa klabu hiyo.
Simba inatarajia kufanya uchaguzi mkuu baada ya viongozi waliokuwa madarakani kumaliza muda wao wa miaka minne kwa mujibu wa katiba.
Hata hivyo, muundo wa uongozi unatarajiwa kuwa tofauti endapo wanachama wa klabu hiyo watapitisha mabadiliko ya baadhi ya vipengele vya katiba yao katika mkutano mkuu utakaofanyika Jumapili kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Kwa sasa Simba iko chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah "Try Again" baada ya Rais, Evans Aveva na Makamu wake, Goefrey Nyange ‘Kaburu' kukabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha. 
Simba ndio mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mwakani itaiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.