Update:

Burundi yalaani kitendo cha serikali ya Canada kuwazuia Warundi kushiriki kura ya maoniWizara ya Mambo ya Nje ya Burundi imekosoa vikali hatua ya viongozi wa Canada ya kuwazuia Warundi wanaoishi katika nchi hiyo kushiriki katika kura ya maoni ya jana na kusema kuwa, kitendo hicho ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Burundi kupitia wizara hiyo imesema kuwa, serikali ya Canada iliwazuia raia wa nchi hiyo kushiriki kura hiyo ya maoni iliyofanyika nchini Burundi Alkhamisi ya jana na katika ofisi za kidiplomasia za nchi tofauti nje ya nchi hiyo ambapo serikali ya Ottawa haikuwaruhusu Warundi kushiriki zoezi hilo, kitendo ambacho kimetajwa na serikali ya Bujumbura kuwa kinakinzana na mikataba yote ya kimataifa.
Rais Pierre Nkurunziza akipiga kura katika uchaguzi wa jana wa kura ya maoni

Hii ni katika hali ambayo Canada imetangaza kwamba haikukubali ombi la ubalozi wa Burundi mjini Ottawa la kufungua kituo cha upigaji kura katika ofisi ya kidiplomasia ya nchi hiyo. Katika radiamali yake, Philippe Nzobonariba,Msemaji wa Serikali ya Burundi amelaani kitendo hicho cha serikali ya Canada. Upigaji kura ya maoni nchini Burundi ulifanyika Alkhamisi ya jana katika anga ya amani. Hata hivyo wapinzani wa serikali wamepinga mpango wa kuitishwa kura hiyo wakisema itamsafishia njia rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza ya kuendelea kusalia madarakani.

source:Parstoday