Update:

Jeshi la Nigeria lawaokoa mateka 149 kutoka mikononi mwa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limewakomboa mateka 149 kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.
Onyema Nwachuku, msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, mateka hao ambao ni wanawake na watoto wamekombolewa baada ya jeshi kushambulia maficho ya wanamgambo wa Boko Haram katika eneo la Yerimari Kura katika jimbo la Borno.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, miongoni mwa waliokombolewa wamo wanawake 54 na watoto 95 ambapo katika operesheni hiyo ya jeshi wanamgambo watatu wa kundi hilo wameuawa na wengine watano kuchukuliwa mateka.
Hayo yanajiri katika hali ambayo kumekuwa na taarifa kwamba, serikali ya Nigeria imekuwa ikifanya mazungumzo na kundi hilo la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kuhusu uwezekano wa kusitisha mapigano, lengo kuu likiwa ni kuhitimisha kikamilifu uadui na uhasama baina ya pande mbili.
Wanamgambo wa Boko Haram wa Nigeria
Mwezi uliopita kundi la kigaidi la Boko Haram liliwaachia huru mabinti 100 kati ya 110 liliowateka nyara mwezi Februari mwaka huu, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Tokea kundi la kigaidi la Boko Haram lianzishe uasi wake nchini Nigeria mwaka 2009, watu zaidi ya 20 elfu wameuawa. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi kutokana na ugaidi wa Boko Haram.
Kwa sasa wigo wa harakati na mashambulio ya Boko Haram umepanuka hadi katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.

No comments