Update:

Watu watatu wauawa katika mapigano ya kusini mwa Libya


Ofisi ya habari ya kituo cha afya mjini Sabha, kusini mwa Libya imetangaza habari ya kuuawa watu watatu katika mapigano mapya yaliyotokea mjini humo.

Ofisi hiyo imesema pia kuwa, mbali na kuuawa watu hao watatu, watu wengine 20 wamejeruhiwa katika mapigano ya jana Jumanne kati ya makabila hasimu mjini humo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu watu 10 wameshauwa katika mapigano mbalimbali tangu mwanzoni mwa mwezi Februari, 2018.

Kwa upande wake, Fayez al Sarraj, waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya amekutana na wakuu wa kijeshi wa kusini mwa nchi hiyo na kuwahimiza watekeleze vizuri majukumu yao.Fayes al Sarraj, waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa LibyaMji wa Sabha wa kusini mwa Libya umekuwa katika hali ya wasiwasi tangu siku ya Jumapili kutokana na mapigano ya kikabila huku ndege za kivita zikiruka muda wote katika anga ya mji huo.

Maafisa wa Baraza la Mji wa Sabha wanasema kuwa, karibu familia 120 zimekimbia nyumba zao kutokana na mapigano hayo.

Libya haijawahi kushuhudia usalama na utulivu tangu mwaka 2011, hususan baada ya Marekani na NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo katika kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi.

Nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika imekuwa uwanja wa mapigano baina ya makundi mbalimbali yakiwemo ya kigaidi tangu wakati huo hadi hivi sasa.