Update:

Wanachuo wanaosomea utabibu wafanya maandamano nchini Tunisia
Wanafunzi wanaosomea taaluma ya udakitari nchini Tunisia wamefanya maandamano nje ya ofisi ya Wizara ya Afya wakishinikiza kutekelezewa matakwa yao.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, wanachuo na wanafunzi walioko katika masomo ya nyanjani wapatao 1,500 wameshiriki maandamano hayo katika mji mkuu Tunis, kuishinikiza Wizara ya Afya kuheshimu haki na matakwa yao.

Hali kadhalika wameitaka serikali kuangalia upya mageuzi yaliyopasishwa hivi karibuni na Wizara ya Afya, yanayotaka kurejeshwa nyuma kwa miaka kadhaa utoaji wa cheti cha diploma kwa wanafunzi wanaosomea utabibu.Polisi wakikabiliana na waandamanaji

Maandamano haya yanajiri katika hali ambayo, Ofisi ya Rais wa Tunisia mapema mwezi huu ilitangaza kwamba, muda wa hali ya hatari umeongezwa nchini humo kwa miezi saba mingine.

Sheria ya hali ya hatari ilianza kutekelezwa nchini Tunisia tarehe 24 Novemba 2015 baada ya kutokea shambulio la kigaidi dhidi ya basi moja la askari wa ulinzi wa Rais mjini Tunis. Sheria hiyo imekuwa ikirefushwa mara kwa mara.