Update:

Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya maji Ngaramtoni-NGAUWSA watakiwa kutimiza ndoto za wananchi za kupata maji safi na salama

Wajumbe wa bodi mpya ya Mamlaka ya Maji Ngaramtoni ( NGAUWSA) wametakiwa kutumiza ndoto za wananchi na wakazi wa Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni kwa kuhakikisha wananchi hao, wanapata maji safi na salama kama sera ya serikali inavyoelekeza. 

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, halmashauri ya Arusha, mheshimiwa Diwani Raymond Lairumbe wakati akifungua semina elekezi iliyotolewa kwa wajumbe hao wa bodi kabla ya kuzinduliwa kwa bodi hiyo na kuanza kazi rasmi. Mheshimiwa Lairumbe amewataka wajumbe hao wa bodi kutumia nafasi waliyopewa na taifa, kupambana na kutatua changamoto za upatikanaji wa maji kwa wananchi wa mji mdogo wa Ngaramtoni tofauti na hali ilivyo sasa. 

Ameongeza kuwa kimsingi, wananchi wa halmashauri ya Arusha, hawakutakiwa kuwa na tatizo la upatikanaji wa maji, kutokana na uhalisia wa vyanzo vya maji vipo ndani ya halmshauri yao.

Aidha mhe. Lairumbe amethibitisha kuwa, ukosefu huo wa maji, unatokana na usimamizi hafifu uliokuwepo wa miradi ya maji iliyokuwepo, uharibifu wa mazingira ya vyanzo vya maji pamoja na usimamizi hafifu wa fedha za watumia maji , hali iliyosababisha kushindwa kufanya matengenezo ya miundo mbinu ya maji. 

Hata hivyo amewataka wajumbe hao, kutumia dhamana waliyopewa, kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na uchangiaji wa gharama za maji kwa ustawi wa miradi ya maji na upatikanaji endelevu wa maji safi na salama. 

" Tumieni muda mwingi kuweka mikakati ya utunzaji wa vyanzo vya maji,uendeshaji na uendelezaji wa miradi ya maji ili wananchi wapate huduma,zaidi usimamizi wa mamlaka ya maji kwa masuala ya fedha ili mapato yatumike kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi" amesema Lairumbe

Meneja wa Mamlaka ya Maji Ngaramtoni - NGAUWSA Clayson Kimaro, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi juu mwongozo wa bodi na majukumu ya wajumbe, pamoja na kufahamu Sera ya maji ya taifa ya mwaka 2029 na sheria na. 12 ya mwaka 2009. Naye Mhandisi wa maji mkoa wa Arusha, Mhandisi Joseph Makaidi, ametaja majukumu ya bodi ni pamoja na kupitisha miradi ya maji, kupitisha bajeti na kudhibiti mapato na matumizi ya NGAUWSA , kutafakari masuala ya kisera kulingana na hali halisi, ili sera ziendane na mabadiliko ya kila wakati na kuwasilisha mapendekezo yote kwa waziri mwenye dhamana.

Naye mwenyekiti wa Bodi ya NGAWSA , ndugu John Sirikwa ameahidi kushirikiana na wajumbe, watalamu wa maji na wananchi ili kuweka mikakati endelevu, itakayowezesha upatikanaji wa maji safi na salama sambamba na utunzaji wa mazingira.

No comments