Update:

Waislamu Uingereza waendelea na kampeni ya kuwapa makazi wasio na nyumba kipindi hiki cha baridi kali

Misikiti mbalimbali katika kona tofauti za Uingereza na Ireland zinaendelea na zoezi lao la kuwapa makazi na chakula watu wasio na nyumba katika kipindi hiki ambapo baridi kali imezikumba nchi hizo mbili.

Vimbunga vya baridi kali vilivyolikumba eneo la mashariki mwa Ulaya kikiwemo kimbunga cha Emma, hadi sasa vimeshababisha watu 60 kupoteza maisha katika eneo hilo wengi wao wakiwa ni wale wasio na nyumba wanaolala mitaani.

Rabnawaz Akbar, mwanaharakati wa misaada ya kibinadamu wa Msikiti wa Makki, kaskazini mwa mji wa Manchester amenukuliwa akisema kuwa, hali ya hewa ni mbaya hivyo tumekaa na kufikiri kwa nini tusifanye jambo jema la kuwasaidia wanadamu wenzetu?Msikiti wa Khizra huko Cheetham Hill pia umekuwa ukitoa huduma mbalimbali za kujitolea kwa watu wenye haja.

Wanaharakati wa jamii hiyo wamekuwa wakibakia misikitini ili kuwahudumia watu wasio na makazi, kuwapa chakula, mahali pa kujisitiri na hata sehemu za kuoga.

Fida Hussain ambaye ni kansela wa mji wa Oldham huko England anasema, Taasisi ya Kiislamu ya Ulaya itaendelea na ratiba zake za kuwasaidia watu wasio na makazi hadi hali ya hewa itakapokuwa nzuri.

Amesema, watu wamekuwa wakifanya mambo mazuri sana. Wote wanashirikiana kuwasaidia wenye haja kiasi kwamba hata madereva wa taxi wamekuwa wakiwafuata na kuwakusanya watu wasio makazi katika sehemu mbalimbali na kuwapeleka misikitini kwa ajili ya kupata hifadhi bila ya kuwalipisha chochote.

Amesema: “Hapa katika mji wa Oldham, watu wa kujitolea wamekuwa wakienda sehemu mbalimbali licha ya hali ya hewa kuwa ya baridi kali na kutafuta watu wasio na makazi na kuwaleta kwenye kituo hiki.”
Baridi kali UingerezaJambo hilo jema limekuwa likifanywa pia na misikiti ya Ireland. Bi Summayah Kenna, mkuu wa kitengo cha ustawi cha Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu huko Ireland anasema: Tuna timu ya kusimamia usalama na kutoa huduma kwa watu hao ili kuhakikisha kuwa maeneo wanakopelekwa kujisitiri yana joto la kutosha hususan wakati wa usiku.

Baadhi ya misikiti huko Ireland hata imekuwa ikiwapa magodoro na mashuka mazito ya kujifunikia watu wanaolala mitaani.

Jamie ni Mkristo ambaye ni katika watu wasio na makazi nchini Uingereza sambamba na kuonesha furaha na kustaajabishwa kwake na miamala hiyo mizuri ya Waislamu amesema, licha ya kuweko propaganda mbaya dhidi ya Waislamu, lakini misikiti ya Uingereza inafanya kazi nzuri sana ambayo mamlaka husika zimeshindwa kufanya.

Amesema: “Waislamu wamenikaribisha vizuri sana, wamenipa kitu cha kula na kunywa. Jambo ambalo mamlaka husika hapa haiwezi kutufanyia.

Zoezi hilo muhimu la Waislamu nchini Uingereza na Ireland limekuja licha ya kuongezeka mashambulizi ya chuki dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada.