Update:

Waasi washambulia nyumba ya Rais Kabila, waua askari mmoja Congo DR


Waasi wa kundi la Mai Mai wameshambulia nyumba ya Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo karibu na mji wa Beni huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuua askari mmoja.

Ripoti zinasema Rais Joseph Kabila hakuwa ndani ya nyumba hiyo wakati iliposhambuliwa na waasi wa Mai Mai.
Shambulizi hilo la waasi limekabiliwa na mapambano makali ya jeshi la serikali lililofanikiwa kuwafurusha wapiganaji hao. 
Waasi wameshambulia nyumba nyingine ya Rais Kabila wa Congo
Shambulizi hilo ambalo ni pili dhidi ya nyumba ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika kipindi cha miezi mitatu ya hivi karibuni ni kielelezo cha kuzorota hali ya usalama kulikosababishwa na hatua ya Joseph Kabila kukataa kuachia madaraka baada ya kumalizika muhula wake wa utawala mwaka 2016.

Nyumba nyingine ya Rais Joseph Kabila ilishambuliwa na kuchomwa moto katika jimbo la Kivu Kaskazini Disemba mwaka jana. Polisi mmoja aliuawa katika shambulizi hilo.