Update:

MFUMUKO WA BEI FEBRUARI 2018 WAONGEZEKA KWA ASILIMIA 4.1



Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi, Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo ofisini kwake, Dar es Salaam.



OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Februari 2018, umeongezeka kidogo hadi kufikia aslilimia 4.1 ikilinganishwa na asilimia 4.0 ilivyokuwa mwezi Januari 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi, Ephraim Kwesigabo, amesema hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Februari 2018 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2018.

Alifafanua kwamba kuongezeka kwa mfumo wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2018 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za vyakula ingawa kuna bidhaa chache za vyakula zilizochangia.



Ameeleza kuwa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kati ya Februari 2017 na Februari 2018 ni pamoja na mkaa, kwa asilimia 17.6, gesi ya kupikia 11.1, mafuta ya taa 9.9, petroli 13.1, dizeli 11.3, huduma za meno 12.9, viatu 3.4, mavazi ya wanaume 3.4 na mavazi ya wanawake 3.8.



Kwa upande mwingine wa hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki alisema ni kama ifuatavyo: Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2018 umepungua hadi asilimia 2.1 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia Januari 2018.



Kwa upande wa Kenya, mfumuko kwa mwaka ulioishia Februari 2018 umepungua hadi asilimia 4.46 kutoka 4.83 kwa mwaka ulioishia Januari 2018.