Update:

HALMASHAURI YA ARUSHA YAVUKA LENGO KWA IDADI KUBWA UPANDA WA MITINa Elinipa Lupembe ,Arusha DC

Katika kuelekea siku ya upandaji miti kitaifa, halmashauri ya Arusha inaadhimisha siku hiyo ikiwa na mafanikio makubwa ya upandaji miti kwa kuvuka malengo kwa mwaka uliopita wa 2017.

Halmashauri imefanikiwa kupanda idadi kubwa ya miti, ukilinganisha na malengo ya kitaifa ya kila halmashauri kupanda miti 1,500,000 kwa mwaka.

Afisa Misitu, halmashauri ya Arusha, Joseph Masawe, amesema kuwa halmashauri imepata mafanikio makubwa katika upandaji miti kwa mwaka 2017, baada ya kupanda miti milioni 2.3 kutoka malengo ya kupanda miti 1,500, 000, sawa na asilimia 158% na ongezeko la asilimia 58%


Hata hivyo Afisa Misitu huyo amethibitisha kuwa, mafanikio hayo yanahamasisha kuendelea kupanda miti mingi zaidi kwa mwaka huu wa 2018 kuliko mwaka uliopita wa 2017, kwa kujikita zaidi kwenye maeneo ya kanda kame.

Masawe ameongeza kuwa mafanikio hayo yamefikiwa baada halmashauri kuwa na kitalu cha miche ya miti, chenye uwezo wa kuotesha miche elfu 50 kwa wakati mmoja na kinatumika kama shamba darasa kwa wakukima wa miti.

Amefafanua kuwa ndani ya kitalu hicho, kunaoteshwa miche ya aina tofauti, zaidi kwa kutegemea hali ya hewa ya maeneo ya halmashauri.

“Ipo miti inayostahimili ukame kwa maeneo ya kanda kame, miti ya maeneo ya vyanzo na kingo za maji inayotunza maji, miti ya nyanda za juu zisizo kame hupandwa miti ya mbao” amesema Masawe.Hata hivyo kupitia kitalu hicho halmashauri inatoa miche ya miti bure, kwenye vijiji vyote, taasisi za serikali na binafsi, pamoja na kwa watu binafsi, wanafika halmashauri na kuchukua aina ya miche wanayohitaji.Pawasa Loishiye mkazi wa kijiji cha Olgilai, alikutwa na mwandishi akichukua miche ya miti kwenye kitalu cha halmashauri amesema kuwa, huduma hiyo inawahamasisha kuotesha miti mara kwa mara kwenye maeneo yao.

Loishiye ameonesha kufurahishwa na kuridhishwa na huduma inayotolewa na halmashauri, kwa kuwa katika vitalu vingine hulazimika kununua mche kwa gharama ya shilingi mia mbili mpaka mia tatu kwa mche, jambo ambalo huwapunguzia gharama hizo kwa kuchukua miche bure,