Update:

Upelelezi kesi ya jinai inayowakabili Susan Kiwanga na Peter Lijualikali umekamilika.

Morogoro. Upelelezi kesi ya jinai inayowakabili wabunge wa Chadema, Susan Kiwanga wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero umekamilika.

Wabunge hao na washtakiwa wengine 41 ambao wote wapo nje kwa dhamana leo Jumatano Januari 31,2018 wamefika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro shauri lilipotajwa.

Katika kesi hiyo mbele ya hakimu Ivan Msacky, washtakiwa wanakabiliwa na makosa manane likiwemo la kuchoma moto ofisi ya serikali ya kijiji na kuharibu mali wanalodaiwa kulitenda Novemba 26,2017 katika kata ya Sofi wilayani Malinyi.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila umesema upelelezi umekamilika.

Gloria ameiomba Mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali ambayo imepangwa Februari 27,2018.