Update:

MVUTANO WA KESI YA SUGU WAJA NA MAJIBU......MAHAKAMA YAAMURU USHAHIDI WA SAUTI KUSIKILIZWA


Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imeamuru ushahidi kusikilizwa ushahidi wa sauti katika kesi inayomkabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi  na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanual Masonga.
Uamuzi huo umetolewa leo mahakamani hapo baada ya mvutano uliotokea jana Jumanne ambapo upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu kuiomba mahakama hiyo kutopokea ushahidi huo kwa madai kuwa  haukidhi matakwa kisheria.
Baada ya uamuzi huo wa kukubali utetezi huo uliotolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite shahidi namba tano katika kesi hiyo upande wa mashtaka Inspekta Joram Magova alitoa ushahidi wa sauti aliyowarekodi Mbilinyi na Masonga kwa kufunga Spika zilizowezesha kusikika kwa ufasaha ndani ya mahakama hiyo.
Awali kabla ya kuanza kesi hiyo ulinzi uliimarishwa katika jengo la Mahakama Kuu Mbeya ambako mahakama hiyo ipo.
Sugu na Masonga wanashtakiwa kwa kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, Desemba 30,2017 katika mkutano wa hadhara walioufanya kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge.
Asubuhi ya leo Jumatano Januari 24,2018 askari waliimarisha ulinzi, huku wakiwazuia wafuasi wa Chadema kuingia katika jengo la Mahakama kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Mwakagenda wameingia katika ukumbi wa Mahakama kufuatilia shauri hilo.
Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite.