Update:

Jinsi ya Kupata Kazi yenye Kipato Kikubwa Zaidi“Nimechoka kufanya kazi hii, Nataka kufanya kazi nyingine” Haya yalikuwa maneno ya kijana mmoja makini aliyetaka kubadilisha kazi ili kupata kazi inayolipa zaidi. Kwa sababu alitamani hivyo, nilimpa ushauri fulani, nikamuuliza kwa upole nikijaribu kuchimba sababu inayomsukuma kubadili kazi. Jibu lilikuwa lile lile ambalo wengi wangelitoa, “nataka kulipwa pesa nyingi zaidi”. Katika kumjibu dakika chache kabla ya kupanda ndege, nilizungumza naye njia tatu ambazo zingemsaidia katika azma yake ya kubadilsha kazi, ambazo naamini zinaweza kukusaidi pia.

1) Fanya zaidi ya unacholipwa,

Jambo la muhimu unalopaswa kulifahamu ni kwamba thamani yako inapimwa kwa mchango wako.  Kadiri unavyozalisha zaidi katika kazi uliyopewa, ndivyo unavyojihakikishia fursa ya kupata kipato zaidi. Kwa hili ni muhimu niseme kuwa unapaswa kutofautisah kati ya kazi uliyopewa na uzalishaji. Kazi ni kile unachokifanya likini uzalishaji ni matokeo ya kile ulichokizalisha. Katika kila kitu unachofanya jiulize swali hili: Je nini matokeo ya jambo ninalolifanya? Watu wenye kaliba ya uzalishaji wa kiwango cha juu wanatambuliwa kirahisi. Ni ukweli usiopingika kuwa wanaopata kazi nzuri, wanazipata kupitia maoni ya wengine walioshuhudia matokeo ya kufanya vizuri katika kazi zao.

2) Ongeza uwezo wako

Moja ya somo nililojifunza kwa vitendo katika maisha yangu ni kuwa; watu watakulipa si kwa sababu ya unachokifanya bali kwa sababu ya wewe ni nani (uwezo unaoonyesha). Si haki kudai ongezeko la mshahara kama hujaongezeka kiuwezo na kiujuzi kwenye kazi yako. Kuomba kazi nyingi sio njia pekee ya kupata kazi nzuri, lakini badala yake jiulize maswali haya:

–   Kazi gani nzuri natafuta?

–    Je uwezo gani ninapaswa kuongeza ili kubadili kazi yangu ya sasa? (mafunzo ya muda mfupi, kupata vyeti vinavyotambuliwa kimataifa nk)

Kadiri unavyoongeza uwezo wako ndivyo unavyokuwa wa kipekee na unafungua milango kwa ajili ya fursa zaidi kwa ajili yako.

3) Dumisha mawasiliano mazuri na mwajiri wako wa sasa. 
Moja ya makosa ambayo watu wengi wamefanya katika maisha yao ni kuharibu uhusiano wao na waajiri wao kwa sababu tu wanataka kuacha kazi. Dunia ni ndogo sana, unaweza kukutana na mtu fulani mahali fulani bila kujua. Njia nzuri ya kuacha kazi yako ya sasa ni kuwa na mahusiano mazuri na utendaji kazi mwema kwa mwajiri wako. Uwe katika ubora wako wa juu unapoacha kazi mahali ili kuacha alama ya ubora mahali hapo na kwenda pengine. Kama utazingatia hilo upo karibu sana kuifikia ndoto ya kupata kazi nzuri zaidi.  Waajiri wengi makini watataka kuwasiliana na mwajiri wako wa zamani ili kupata maoni juu yako; Cheza kwa akili.