Update:

George Weah aapishwa urais wa Liberia LeoNyota wa zamani wa kandanda duniani George Weah ameapishwa leo na kuwa Rais wa Liberia katika sherehe iliyohudhuriwa na maelfu ya watu katika mji mkuu, Monrovia.

Weah amechukua nafasi ya rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuchaguliwa kuongoza taifa la Afrika, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye amestaafu.

Sherehe hiyo imehudhuriwa na viongozi wa mataifa kadhaa pamoja na nyota wa kandanda duniani.

Akihutubia baada ya kula kiapo, Rais Weah amesema kuwa: "Nimekuwa katika viwanja vingi maishani, lakini sijawahi kuwa na hisia hii niliyonayo leo."

Rais huyo mpya wa Liberia ameahidi kujitolea kuwatumikia raia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Amesema: "Nitafanya zaidi ya mchango ninaotarajiwa kutoa ili kutimiza matarajio yenu, lakini naomba nanyi mtimize matarajio yangu, siwezi kutimiza haya peke yangu."George Weah, Rais mpya wa Liberia

Rais mpya wa Liberia ameahidi pia kwamba, atapambana na ufisadi na kuchukua hatua za kuboresha uchumi wa nchi hiyo masikini.

Weah alicheza mpira wa miguu katika klabu kadhaa za Ufaransa na Uingereza miaka ya 1980 na 1990 na akaibuka Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya Fifa ya Mchezaji Bora wa mwaka duniani.

Weah aliingia katika siasa baada ya kustaafu soka mwaka 2002 na akawa miongoni mwa maseneta katika Bunge la Liberia.

Aligombea urais mwaka 2005, na alimshinda Bi Johnson Sirleaf wakati wa duru ya kwanza katika uchaguzi huo, lakini akashindwa katika duru ya pili ambapo kambi yake ilisusia kushiriki katika duru ya pili.