Update:

DHAMANA KESI YA UHUJUMU UCHUMI KUJULIKANA FEBRUARI 5 MWAKA HUUMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imesema Februari 5, mwaka huu, itatoa uamuzi dhidi ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabiki Mkurugenzi wa Kampuni ya Lucky Shipping Co.Ltd , Issa Haji( 39) na wenzake Abdallah Issa Hanga( 73), kama watapata dhamana au la.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, amesema hayo leo baada ya upande wa utetezi kuwasilisha maombi mahakamani hapo wakitaka washtakiwa hao kupewa dhamana.Wakili wa utetezi, Dismas Raphael amewasilisha maombi hayo akipinga hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), aliyewasilisha hati ya kuzuia ya dhamana ya washtakiwa akidai hati hiyo ya haijafafanua ni kwa namna gani usalama na maslahi ya Taifa yatazurika endapo washtakiwa watapewa dhamana, hivyo wanahoji uhalali wa DPP kumnyima mtu dhamana bila kufafanua misingi yake.

Awali, wakili wa Serikali Simon Wankyo alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa wakipewa dhamana, wataingilia maslahi ya Taifa na kuiomba Mahakama ijielekeze katika suala hilo.Wakili Wankyo aliiomba Mahakama itupilie mbali hoja za upande wa utetezi kwa sababu hazina msingi.

Baada ya mabishano ya kisheria ya pande zote mbili, kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 5 Mwaka huu, kwa ajili ya uamuzi kama washtakiwa watapata dhamana au la.Washtakiwa wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa uhalifu kinyume na sheria.

Katika hati ya mashtaka ilidaiwa, kati ya Julai 19,mwaka 2017 na Januari 16, mwaka 2018 jijini Dar es Salaam, walitoa ushauri, msaada na maelekezo katika kutenda kosa la jinai la mtandao wa uhalifu ambalo ni kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye meli iitwayo Huihang 68 zamani ilijulikana kama Greko 02, bila kuwa na hati ya usajili kutoka kwa msajili wa meli nchini kwa lengo la kujipatia faida kutoka katika shughuli za uvuvi haramu.

Pia kati ya Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu, washitakiwa hao huku wakifahamu kuwa ni kosa kisheria waliruhusu upeperushwaji wa bendera katika meli hiyo bila kuwa na leseni kutoka kwa msajili wa meli kwa lengo la kuifanya ionekane kuwa ya Tanzania wakati si kweli.