Update:

Libya kuwaadhibu wanaohusika na biashara ya utumwa


Serikali ya Libya imesema itawaadhibu wale wote watakaopatikana na hatia ya kuhusika na biashara ya utumwa na udhalilishaji wa wahajiri wa Kiafrika

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu wa Libya Bw. Ahmad M'etig, ambaye ameongeza kuwa, yeyote anayehusiana na ukiukaji wa haki za wahamiaji haramu nchini Libya ataadhibiwa na serikali.

Hivi karibuni kulienea ripoti kuhusu minada katika sehemu mbalimbali nchini Libya ambapo wahamiaji wa Afrika waliuzwa kama watumwa kwa dola 400 za Kimarekani.

Bw. Metig amesema, tume ya kuchunguza matukio hayo imeundwa nchini Libya. Pia amesisitiza kuwa mateso na uuzaji wa binadamu ni vitu vilivyopigwa marufuku nchini Libya na katika nchi za Kiislamu.Watumwa wakishikiliwa nchini Libya

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mnada huo wa kuwauza Waafrika kama watumwa nchini Libya ni uhalifu dhidi ya binadamu

Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 baada ya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kuingia kijeshi huko Libya katika kampeni ya kumng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Tangu mwaka huo hadi hivi sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kushuhudia usalama na utulivu hata mara moja.