Update:

VIFARANGA VYA THAMANI YA TSH. 12.5 MILIONI MALI YA MARY MATIA MKAZI WA MIANZINI ARUSHA KUTEKETEZWA NA MOTOVifaranga vya kuku 6,400 vya chomwa moto baada ya kunaswa vikiingizwa nchini kupitia Longido mkoani Arusha. Vifaranga hivyo vilikamatwa juzi vikitokea nchini Kenya.

Taarifa zinasema thamani ya vifaranga hivyo ni Sh12.5 milioni na ni mali ya mfanyabiashara Mary Matia (23) mkazi wa Mianzini jijini Arusha anayeshikiliwa na polisi.

Akizungumza katika mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Namanga, ofisa mfawidhi wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Kaskazini, Obedi Nyasembwa alisema tangu mwaka 2007 Serikali ilipiga marufuku kuingiza mayai na vifaranga kutoka nje ya nchi. Alisema uamuzi huo wa Serikali ulichukuliwa ili kudhibiti magonjwa ya mifugo ukiwamo wa mafua ya ndege.

Akizungumza akiwa chini ya ulinzi wa polisi, mfanyabiashara Matia alikiri kuingiza nchini vifaranga hivyo akisema hakuwa akijua kama uingizaji umepigwa marufuku.