Update:

UTATA KIFO CHA MTUHUMIWA WA UJAMBAZI ROBERT MASSAWE

Mkazi wa Dar es salam Robert Massawe anaedaiwa kuwa ni jambazi sugu amedaiwa kuuawa katika mazingira ya kutatanisha wakati akitoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuwabaini wanao daiwa kuwa ni washiriki wenzake katika matukio ya ualifu

Hata hivyo, wananchi wa eneo linalodaiwa kulikuwa na majibizano ya risasi wamedai kutosikia milio huku baadhi ya viongozi wakisema wamepokea taarifa tu kutoka polisi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, amesema ofisini kwake kuwa Massawe alikamatwa jijini Dar es Salaam pamoja na mkewe ambaye hakumtaja jina lake kwa sababu za kiusalama.

Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na simu 19 za mkononi zilizodaiwa kuibwa katika matukio mbalimbali ya mauaji mkoani Kilimanjaro, betri tisa za simu za mkononi na laini 58 za simu za mtandao wa Vodacom zipatazo 58 na waliamua kumsafirisha hadi Kilimanjaro kwa msaada wa simu alizokuwa akitumia.

“Baada ya kubainika kuwa mtu huyo amefanya matukio mengi mkoani Kilimanjaro ndipo tulipoamua kumsafirisha hadi hapa ili atupatie ushirikiano wa kubaini sehemu zilipo silaha wanazozitumia katika matukio mbalimbali pamoja na washiriki wenzake,” alisema Kamanda Issah.

Alisema Massawe baada ya kufikishwa Kilimanjaro, aliendelea kutoa ushirikiano kwa polisi na aliwapeleka katika eneo la Kaloleni liliko dampo la kuputa taka kisha kufukua katika moja ya eneo na kutoa bunduki aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 2761 iliyokuwa imefukiwa chini ikiwa na risasi 24.
Kamanda Issah alisema kwa mujibu wa kumbukumbu ya maganda ya risasi yaliyokuwa yakiokotwa katika matukio mbalimbali ya ujambazi na mauaji, inaonekana kuwa bunduki hiyo ndiyo iliyokuwa ikitumika.

Alisema mtu huyo aliliambia Jeshi la Polisi kuwa baadhi ya washiriki wenzake wanapatikana Holili wilayani Rombo karibu na kiwanda cha saruji cha Moshi na kwamba Oktoba 08, mwaka huu, majira ya saa 10 alfajiri, waliamua kwenda na mtuhumiwa huyo kwa ajili ya kwenda kuwaonyesha.

“Mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu, walipofika katika eneo hilo akiwa amesimama ndipo alipoanza kupiga kilele kwa kusema polisi wapo eneo hilo hali iliyosababisha majambazi hao kukimbia huku wakiwa wanapiga risasi ovyo katika harakati za kujihami wasikamatwe,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema askari walianza kutupiana risasi na majambazi hao, ndipo walipogundua kuwa mhalifu waliyekuwa naye amejeruhiwa na risasi sehemu ya mkono wa kushoto, mgongoni na mguu wa kulia hali iliyosababisha kifo chake.

Akijibu swali la wanahabari kuhusi ni nani aliyempiga risasi mhalifu huyo aliyeonyesha kuwa muwazi kwa Jeshi la Polisi na kutoa ushirikiano, Kamanda Issah alisema hana uhakika ni nani aliyempiga risasi ila walichogundua ni mtuhumiwa huyo kujeruhiwa kwa risasa zilizosababisha kifo chake.Aidha Kamanda Issah alisema Massawe alikiri kushiriki katika matukio mbalimbali na kwamba mwaka 1991 na 1992 aliwahi kukamatwa Tarakea wilayani Rombo kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kumbukumbu zingine alizokiri kuhusika ni tukio la Juni 26, 2012 katika maeneo ya Kiusa jirani na kituo cha mafuta cha Panone kwa kumvamia mfanyabiashara mmoja na kupora fedha.

Tukio lingine alilokiri ni la Septemba 29, 2014 walimvamia mfanyabiashara aitwaye Robert na kumpora fedha pamoja na vocha za simu.

Alisema kumbukumbu zingine ni Juni 26, 2015 walipovamia maeneo ya Holili Stendi wilayani Rombo na kupora fedha kwa mfanyabiashara mmoja na kuwaua watu wawili. Pia alisema Aprili 3, mwaka huu, walimvamia mfanyabiashara maeneo ya Himo na kumpiga risasi ya paja kisha kupora Sh. milioni sita.

Matukio mengine aliyoshiriki ni la Juni 26, mwaka huu katika maeneo ya Woodland walipomvamia mfanyabiashara na kumpora simu na vocha na Julai 22, mwaka huu maeneo ya Mailisita High Way Supermarket walipomvamia mfanyabiashara na kumpiga risasi ya paja kisha kupora simu na vocha za simu.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma wilayani Rombo huku mke wa marehemu huyo akiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo,


Mwenyekiti wa kijiji Cha Holili Mjini, January Lyimo, alisema hana taarifa ya tukio la mashambulizi ya risasi katika kijiji hicho.
“Risasi si kitu kidogo, kama kungekuwa ufyatuaji wa risasi lazima tungesikia lakini hakuna kitu kama hicho,” alisema Lyimo.Naye mtendaji wa kata Alfrad Faustine alisema hana taarifa za mauaji yaliyofanyika katika kata hiyo huku akilitaka jeshi la polisi kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi walioko katika kata hiyo.

“Ni kweli kata yetu ipo mpakani na wahalifu wanaweza kutumia kama mwanya wa kutorokea au kufanya mambo yasiyofaa ila wenzetu jeshi la polisi tushirikiane ili kutokomeza uhalifu na si kufanya kimya kimya,” alisema Faustine.

Kwa upande wake, Diwani wa kata hiyo, Williard Assenga, alikiri kupewa taarifa hizo na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Holili kwa kuwa hakuwapo siku ya tukio.
CREDIT:NIPASHE