Update:

MTOTO WA MIEZI MITANO ALIWA NA FISI KATA YA MAKURU WILAYA YA MANYONI MKOA WA SINGIDANA; JUMBE ISMAILLY – SINGIDA
MTOTO mwenye umri wa miezi mitano,mkazi wa Kijiji cha Msemembo,kata ya Makuru,wilayani Manyoni,Mkoani Singida amepoteza maisha baada ya kuvamiwa na fisi anayedhaniwa kuwa na kichaa akiwa amebebwa mgongoni na mama yake mzazi na kisha kuliwa mwili mzima na kubakizwa kichwa.

Kituo hiki kilitembelea katika Hospitali ya wilaya ya Manyoni na kumkuta mama wa mtoto huyo akiwa amelazwa katika wodi ya majeruhi baada ya kushambuliwa na kisha kuumwa mikononi,miguuni na usoni na fisi anayedhaniwa kuwa na kichaa na hivyo kumsababishia majeraha makubwa.


Akizungumza akiwa amelala kitandani kwenye wodi ya majeruhi,Mwanamke huyo,Bi Amina Njiku(42) mkazi wa Kijiji cha Msemembo amefafanua kwamba siku ya tukio majira ya saa tatu asubuhi alikuwa akitokea kufanya biashara zake katika Kijiji jirani cha Mwanjare.


Amesema wakati akirudi nyumbani kwake akiwa njiani,ndipo ghafla alikutana na fisi huyo ambaye baada ya kukea alimrukia na kuanza kumshambulia.


Hata hivyo ameweka bayana mama huyo kuwa baada ya fisi huyo kumrukia alimpigiza chini na kuanza kumng’ata na ndipo alianza kupiga yowe kuomba msaada wa kusaidiwa bila mafaniko hadi kichanga chake kilipoanguka chini na fisi huyo kukitafuna mwili mzima na kubakia kichwa peke yake.


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Manyoni,Dk.Mlewa Ainea amethibitisha kumpokea mwanamke huyo akiwa na hali mbaya sana kutokana na kutokwa na damu nyingi.


Mganga mfawidhi huyo wa Hospitali ya wilaya amesema walipompokea majeruhi huyo walibaini kuwepo majeraha kwenye sehemu mbali mbali za mwili wake ikiwemo kutafunwa vidole vya mikono yote, miguuni na usoni na fisi anayedhaniwa kuwa na kichaa na hivyo kumsababishia majeraha makubwa.


Kutokana na tukio hilo ambalo ni la pili kutokea wilayani Manyoni baada ya lile la kwanza lililotokea Kijiji cha Kintanula,Mganga Mfawidhi ametumia fusa hiyo kutoa wito kwa jamii ya wilaya hiyo kuchukua tahadhari kwenye maeneo yaliyo na wanyama wanaonyesha dalili za kuwa na kichaa.


Dk.Ainea hata hivyo amewataka pia wafugaji wa mbwa wajitahidi kuwadhibiti wazizurure ovyo na wawapeleke kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa kichaa kwani endapo wasipochanjwa upo uwezekano wakakimbilia porini na kuwauma fisi ambao nao huambukizwa na hivyo nao huvamia kwenye makazi ya watu na kuanza kuwashambulia.


Hili ni tukio la pili kutokea wilayani Manyoni baada ya tukio la awali lililotokea katika Kijiji cha Kintanula ambapo wataalamu walifanikiwa kumtibu majeruhi na kuokoa maisha yake.

No comments