Update:

Manispaa Moshi yajitosa bomoabomoa Pasua

Sakata la ubomoaji wa makazi ya wananchi wanaodaiwa kuvamia miundombinu ya reli limechukua sura mpya baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira taarifa ya uhalali wa waliojenga katika maeneo hayo.

Taarifa hiyo inaonyesha maeneo yaliyowekewa alama X na uhalali wa watu kwenye maeneo hayo huku ikibainisha baadhi ya wakazi walijenga katika viwanja halali. Septemba 14, Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) iliweka alama X na kuwataka wamiliki zaidi ya 90 katika eneo la Pasua kitalu JJJ kubomoa majengo yao wakidaiwa kuvamia eneo la reli.

Katika taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo, Michael Mwandezi wananchi waliopo kwenye viwanja hivyo waligawiwa kihalali na wanakaa kihalali. Hata hivyo, manispaa hiyo imependekeza kufanyika kwa mazungumzo kati yake na Rahco kwa lengo la kupata muafaka wenye tija ili kutatua mgogoro huo kabla ya kumalizika kwa notisi ya siku 30.

 Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mchoro wa mipango miji namba 4/138/1162K ulioandaliwa mwaka 1962 na kuidhinishwa na wizara mwaka 1997, ulitenga eneo jirani na kitalu hicho kuwa la viwanda. “Katika mchoro huo ikapendekezwa ipite reli eneo hilo la viwanda kwa ajili ya kutoa huduma kwenye viwanda,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ambayo inadai hata hivyo eneo lote limevamiwa na kujengwa makazi. Taarifa hiyo inaeleza kuwa mwaka 1982, eneo hilo lilipimwa kama la viwanda kwa upimaji wenye usajili namba 19950 ulioidhinishwa na wizara na kugawiwa kwa wawekezaji 45 tofauti tofauti.

 Hata hivyo, tangu wakati huo hakuna kiwanda hata kimoja kilichojengwa na eneo hilo lilivamiwa na kuendelezwa na wananchi kiholela kwa kujenga nyumba za makazi ya kudumu bila kuwa na hati. Mwaka 2002, Manispaa ya Moshi iliandaa rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya matumizi ya ardhi kutoka viwanda na kuwa na makazi, na mapendekezo hayo kuridhiwa na Wizara ya Ardhi. Mwaka 2004, wizara iliidhinisha michoro ya mipango miji namba MMC/MISC/62/0104 na MMC/MISC/63/0104 na mwaka 2008 ikaidhinisha mchoro namba MMC/MISC/136/0108.

Kulingana na taarifa hiyo, michoro hiyo ilipendekeza eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya kujenga reli libadilishwe matumizi kwa kuwa reli hiyo ilikuwa haijajengwa na haiwezi tena kupita eneo hilo. Baada ya kupimwa na kuidhinishwa na wizara kwa ramani ya upimaji yenye usajili namba 39784 wa 2004, namba 60925 wa 2009 na namba 62414 wa 2010, eneo hilo lilipimwa viwanja 90.

Mwanasheria atoa ufafanuzi Akitoa maoni yake kuhusu sakata hilo, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Frank Mushi alisema kwa uso wa kisheria wananchi hao wana haki zote kwa vile waligawiwa viwanja na mamlaka halali. “Hili la Pasua lina sura tofauti sana na wale waliopo mita 15 kwa mjini na mita 30 kwa vijijini ndani ya hifadhi ya reli.

Hapa ni mamlaka ya Serikali ilibadili matumizi ndio wananchi wakagawiwa,” alisema. Wakili huyo alisema endapo sasa kuna ulazima wa Serikali kulitwaa tena eneo hilo, sheria iko wazi kuwa wananchi hao watalazimika kufidiwa na kupewa muda wa kutakiwa kuondoka.

Tayari Mghwira amemuagiza Mwandezi na timu yake kukutana haraka na Rahco ili kuangalia uwezekano wa kuepusha wananchi wasio na hatia katika eneo hilo kubomolewa nyumba zao. Alipoulizwa kuhusu maandalizi ya mazungumzo hayo jana, Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya alisema mchakato umeanza na huenda wakakutana na Rahco wiki hii.

Kuhusu wananchi wa Arabika na Miembeni ambao nao wamewekewa alama X, taarifa hiyo imesema haikugawa eneo hilo kama ilivyo Pasua JJJ, bali wananchi wenyewe ndio walioomba wamilikishwe. “Halmashauri ililazimika kuandaa mchoro wa eneo hilo lililokuwa limeendelezwa kiholela ili kurasimisha makazi.

 Mwaka 2014 Mchoro namba 4/138/1162FA uliidhinishwa na Wizara ya Ardhi” inasema taarifa hiyo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwaka 2017, baadhi ya wananchi waliopimiwa waliwasilisha maombi ya kumilikishwa viwanja hivyo kisheria na kwamba idadi ya viwanja hivyo ni 23. Taarifa hiyo inasema kati ya wamiliki hao wa viwanja 23 walioomba kupatiwa hati za umiliki, viwanja 13 ndivyo vilikuwa vimelipiwa gharama za maandalizi ya hati na 10 vilikuwa havijalipiwa.