Update:

MAELEZO YA MUSHUMBUSI AKIWA CANADA KUHUSU MAUWAJI YA KANUMBAAskari katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam, Sajenti Nyagea amefika Mahakamani Kuu na kusoma maelezo ya Josephine Mushumbusi katika kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili msanii wa fani ya uigizaji filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu.

Mushumbusi katika maelezo hayo alisema Steven Kanumba alikuwa akifanya mazoezi ya kutanua misuli na alimshauri kuyaacha. Pia, alimweleza kuwa anasumbuliwa na maumivu ya moyo.

Lulu ambaye yupo nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi ya kumuua bila ya kukusudia msanii wa filamu, Kanumba. Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2012, nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.

Mbele ya Jaji Sam Rumanyika, Sajenti Nyagea leo Jumatano Oktoba 25,2017 amesoma maelezo ya Mushumbusi aliyoyatoa polisi. Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha Lulu katika kesi hiyo aliieleza Mahakama kuwa Mushumbusi hapatikani kwa kuwa yuko nchini Canada, hivyo aliomba maelezo yake yapokewe kama sehemu ya ushahidi.

Katika maelezo hayo yaliyorekodiwa na Sajenti Nyagea, Mushumbusi alieleza alikuwa na kituo cha tiba mbadala na alikuwa akimtibu Kanumba.

Ameeleza Kanumba alikuwa akisumbuliwa na matatizo mbalimbali na wakati akimhudumia alibaini alikuwa akifanya mazoezi ya kutanua misuli na alimshauri kuyaacha. Mushumbusi katika maelezo hayo anasema Kanumba alimweleza alihisi kuwa na maumivu ya moyo na alimuomba ampe ushauri.

Katika maelezo hayo, amesema siku Kanumba alipokwenda kwake alikuwa na watu wengi, hivyo alimuomba apange siku nyingine na kabla ya kuonana alisikia kuwa amefariki dunia. Upande wa utetezi umefunga ushahidi wake na kesho Oktoba 26,2017 wazee wa baraza watatoa maoni yao.

Credit :Mwananchi

No comments