Update:

FBI: Aliyefanya mauaji ya Las Vegas hana uhusiano na magenge ya kigaidi

Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI imesema Stephen Paddock, ambaye alitekeleza mauaji ya makumi ya watu katika shambulizi la Las Vegas nchini humo hana uhusiano wowote na magenge ya kigaidi.

Kadhalika maafisa wawili wa ngazi za juu wa serikali ya Washington ambao hawakutaka majina yao yatajwe wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa mtu huyo aliyekuwa na umri wa miaka 64 alikuwa na mafungumano au mawasiliano na kundi lolote la kigaidi la kimataifa.

Wakati huo huo, Eric Paddock, ndugu ya Stephen Paddock amenukuliwa na kanali ya televisheni ya CBS News akisema kuwa, "Ndugu yangu hakuwa na mafungamano yoyote na masuala ya dini wala siasa, alikuwa mcheza kamari na mtu wa anasa baada ya kustaafu, hatuelewi vipi aliweza kumiliki silaha zote hizo hatari. Tunahisi kama jabali zito limetuangukia sisi watu wa familia yake."Eneo la tukio Las Vegas

Hii ni katika hali ambayo, vyombo vya habari vya Magharibi vimenukuu tovuti ya propaganda ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) iliyodai kuwa, Stephen Paddock alikuwa mshirika wao na kwamba alitekeleza shambulizi hilo la Las Vegas kwa niaba yao.

Watu wasiopungua 59 wamethibitishwa kuuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya Jumatatu alfajiri karibu na eneo la Mandalay Bay katika mji wa anasa wa Las Vegas nchini Marekani.

Paddock anaripotiwa kujiua baada ya kutekeleza ukatili huo dhidi ya umati mkubwa wa watu waliokuwa katika uwanja wa barudani.

No comments