Update:

Dr. Kigwangallah Asimulia Alivyopokea Uteuzi wa Rais Magufuli


Aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla ameeleza namna alivyopata taarifa za uteuzi wa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.


Dk Kigwangalla kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram amesema Jumamosi alikuwa ziarani Kituo cha Afya cha Kilimarondo wilayani Nachingwea mkoani Lindi.


Amesema siku hiyo saa nane mchana ndipo alipopata ujumbe wa kuteuliwa kushika wadhifa huo mpya.


Rais John Magufuli Jumamosi alitangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.


Dk Kigwangalla amesema, “Baada ya kumaliza kazi kituoni hapo na kuanza ku-rake njia ya kuelekea Liwale, Kituo cha Afya Kibutuka, ndipo mwenyeji wetu anaarifiwa na watu wa Liwale kuwa itakuwaje? Mheshimiwa ataendelea na ziara huku amebadilishiwa majukumu?”


Katika ujumbe huo, Dk Kigwangalla amesema, “Kilimarondo hakuna mtandao zaidi ya TTCL. Ni kilomita takriban 100 za vumbi kuelekea ndani huko. Ni tarafa ya pembezoni kweli kweli. Ni mahala ambapo Nachingwea inapakana na Tunduru.”


Amesema baada ya kupata taarifa hiyo kila kitu ilibidi kisimame papo hapo.


“Namba za NWAMJW (Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto) ilibidi ziondolewe na safari ya kutoka huko ianze! Nimepokea salamu nyingi za pongezi na shukrani kwa Mungu aliye juu. Sitoweza kumjibu kila mtu, uungwana ni kutambua pongezi zenu na dua tele mlizotuombea, nawashukuru sana ndugu zangu. Tuzidi kuombeana dua tu,” amesema.


Dk Kigwangalla amesema wana kazi ngumu ya kukimbia kukidhi matarajio ya kiongozi mkuu aliyewaamini na matarajio ya wananchi.


“Binafsi nawaahidi nyote kuwa sitowaangusha! Ahsanteni sana ndugu zangu, natarajia ushirikiano wenu wa kila hali,” amesema.

No comments