Update:

Zitto, Spika Ndugai hapatoshi

Dar/Dodoma. ‘Hapatoshi’ kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, wakati mmoja akitumia mhimili huo kujibu na kumuonya mwenzake, mwingine amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe wake.
Jana, Ndugai aliliambia Bunge kwamba anaweza kumzuia mbunge huyo asizungumze bungeni kwa muda wote uliobaki na hana cha kumfanya tamko ambalo Zitto amenukuliwa katika akaunti yake ya Twitter akilijibu kwa kusema kuwa Spika huyo ameibua mashtaka yake ili kufunika ufuatiliaji wa wananchi kuhusu hali ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
“Nimegundua Spika Ndugai ameibua mashtaka yangu ili kufunika ufuatiliaji wa wananchi kuhusu Lissu kupigwa risasi. Nimeamua sitawapa hilo.” Mtifuano baina ya Spika Ndugai na Zitto ulianza baada ya kiongozi huyo wa ACT – Wazalendo kusema kwamba Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti mbili za kamati ya Bunge za almasi na Tanzanite.
Mbali na shutuma hizo, mbunge huyo alindika katika akaunti yake ya Twitter kwamba, “Hatujawahi kuwa na Spika anayedhalilishwa na Rais kwamba aliuliza wajumbe gani awaweke kamati za uchunguzi za Bunge.” Kutokana na kauli hizo, Spika Ndugai aliagiza mbunge huyo ahojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku akimshtaki kwa wapigakura wake akisema licha ya kwamba mbunge wao yupo nchini hajafika bungeni kuwawakilisha na yeye (Spika), hana taarifa.
Baada ya Spika Ndugai kutoa mwongozo huo, baadaye jioni Zitto aliandika tena katika akaunti yake hiyo maneno kadhaa ikiwamo; “Bunge la 11 halitii mshawasha. Ndugai anajua namna Bunge la Tisa na 10 lilivyokuwa. Hata kamati hazina kazi. Zakutana wiki moja tu siku hizi.” “Kwenye mazishi ya Spika wa Watu Mzee Sitta, Ndugai aliomba afike japo robo ya Sitta. Hajafika hata asilimia 10 ya Anne Makinda miaka miwili sasa.” “Wabunge wazoefu tulikuwa na matumaini makubwa na Spika Ndugai tulimpigania dhidi ya njama za kumhujumu kutoka Ikulu.
Anatuangusha” Pia Zitto aliandika; “Spika Ndugai amekuwa Spika wa kwanza katika historia ya nchi yetu kushuhudia mbunge anapigwa risasi Mkutano wa Bunge ukiendelea.” Baada ya kauli hizo, ndipo jana Spika Ndugai alipolitangazia Bunge kwamba Zitto apelekwe kwa mara ya pili katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuhojiwa kwa kulidharau Bunge.
Akizungumza mara baada ya kipindi cha maswali na majibu Spika Ndugai alisema anaweza kulichambua Bunge kwa sababu alikuwapo katika vipindi hivyo na Makinda na marehemu Sitta ni walimu wake. “Hawa ni watu nawaheshimu sana na wamenilea sana na ni sehemu ya nilipofika hapa leo.
Utanilinganishaje mimi na milima mikubwa kama Kilimanjaro? Hata siku moja sikio haliwezi kuzidi kichwa,” aliongeza. Alisema katika Bunge la Tisa, Zitto aliwahi kupeleka hoja ya mgodi wa Buzwagi ambayo ilikataliwa na Bunge lakini ikazuka hoja ya kimaadili ambako alihukumiwa hapohapo.
“Alihukumiwa hapohapo akapigwa miezi mitatu. Mnataka niende mkuku mkuku kama lile la Bunge la Tisa nifanane na Mzee Sitta? Hilo pia naliweza kwa nini mnaalika matatizo nashangaa unapambana na Spika,” alihoji. “Nina uwezo wa kumpiga marufuku kuzungumza hadi miaka yote mitano iishe hauna pa kwenda, hakuna cha swali, nyongeza wala kuzungumza utanifanya nini?” alisema Spika Ndugai na kumtaka mbunge huyo kupambana na mtu mwingine lakini sio yeye. “Kwa haya ya Spika sina sababu nayo lakini ya kulidharau Bunge hayo sitaweza kuyavumilia nitalinda mhimili huu kwa nguvu zangu zote.”

No comments