Update:

Polisi watumia mabomu ya machozi kuwatawanya Wafuasi wa Raila Odinga na Uhuru Kenyatta


Polisi wamelazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa vyama vya Jubilee na muungano wa upinzani wa Nasa baada ya kuzua vurugu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) zilizoko jengo la Anniversary Towers.


Wafuasi wa Nasa waliokuwa wakiimba nyimbo “Chiloba lazima ang’oke” walikabiliwa na wafuasi wa Jubilee waliokuwa wakiimba “Tunataka amani”. Makundi yote mawili yalitimua mbio baada ya polisi wa kuzuia ghasia kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.


Huku wakikohoa na wakitafuta mahali salama, wote walikimbia kukwepa kukamatwa.


Maandamano hayo yamefanyika kuitikia wito uliotolewa jana na kiongozi mkuu wa Nasa Raila Odinga kwamba wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kuandamana hadi kwenye makao makuu ya IEBC lengo likiwa kumtoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC Ezra Chiloba kwa madai ya kuhusika kuvuruga uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.


Maandamano hayo yanafanyika siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.


Katika mji wa Kisumu, ambao unatajwa kuwa moja ya ngome za Nasa baadhi ya wakazi waliandamana hadi ofisi za IEBC na baada ya kufika walitoa wito maofisa wa ngazi za juu akiwemo Ezra Chiloba wajiuzulu.


Walimshutumu Chiloba na kikundi chake kwa kufanya njama za kuingilia mchakato wa uchaguzi mkuu ambao matokeo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta yalifutwa na Mahakama ya Juu.


Waandamanao waliokuwa wamebeba matawi ya miti, mabango huku wakipiga yowe na honi za pikipiki walianzia barabara ya Obote wakaenda mtaa wa Oginga Odinga kabla ya kuchukua Barabara Kuu ya Kenyatta na baadaye Mtaa wa Ang’awa katikati ya jiji.

No comments