Update:

Mwanri ategua mgogoro wa wafanyakazi 11 wa kampuni ya Seytun

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amefanikiwa kumaliza mgogoro kati ya waliokuwa wafanyakazi 11 wa Kampuni ya Ujenzi ya Seytun iliyokuwa ikipanua Uwanja wa Ndege wa Tabora na wamiliki wake juu ya kulipwa madai ya malipo ya muda wa ziada na mapunjo ya mishahara.

Mgogoro huo ulimalizika jana mjini Tabora baada ya Wamiliki wa Kampuni hiyo kukubali na kulipa madeni ya wafanyakazi wake ambapo  malipo yalifanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mkuu wa Wilaya ya Tabora.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuamuru kuwang’anywa Hati za kusafiria za viongozi wake wawili wa Kampuni hiyo na kuzuiwa kwa vifaa vyake vya  ujenzi baada ya kuonekana kuwa anataka kuondoka bila kulipa malipo ya wafanyakazi hao.


Akizungumza mara baada ya Kampuni hiyo kuwalipa waliokuwa  wafanyakazi wake Mwanri alisema kuwa amelizika na kazi iliyofanyika na hivi sasa wanaweza kuchukua hati zao za kusafiria na wako huru kuondoa vifaa vyao vya ujenzi kwa sababu wamemalizana na watumishi hao bila kinyongo.