Update:

JE? UNAFAHAMU DUNIA INAKUAMBIA NINI? Hebu angalia haya uone jinsi dunia inakuhadaa;

Kipato chako hakitoshelezi matumizi yako, dunia inakuambia nini? Usiwe na shaka, chukua mkopo na utalipa tu baadaye. Na mamilioni ya watu wanafanya hivyo. Sasa hebu tutafakari pamoja rafiki, kama kipato hakitoshi, dawa ni kuchukua mkopo au kuongeza kipato chako? Unaweza kuona namna dunia inahadaa wengi.

Mtu ana uzito ambao umepitiliza, ambao ni hatari kwa afya yake. Na wote tunajua sababu za uzito kupitiliza ni zipi, kula vyakula isivyo kiafya na kukosa mazoezi, hasa kwa wale ambao kazi zao ni za kukaa siku nzima. Lakini dunia inakuambia nini kwenye hilo? Kama una uzito uliopitiliza basi meza kidonge, ukishameza tu hicho kidonge uzito wote unapungua. Hebu angalia hapo rafiki, wewe ule hovyo, usifanye mazoezi, halafu umeze kidonge na uzito upotee. Halafu uendelee na maisha yako kama ulivyozoea! Unahitaji kuwa makini sana na hii dunia, la sivyo hadaa kama hizi hazitakuacha salama.

Twende kwenye vyombo vya habari na njia nyingine zinazotumika kupashana habari. Angalia kuhusu mafanikio ya watu yanayoandikwa kwenye vyombo hivi. Utaona kote kinachoandikwa ni matokeo ya watu hao. Alianza kuuza nyanya sasa hivi ana kiwanda. Alitokea familia masikini sasa hivi ni bilionea. Aliacha shule sasa hivi ameajiri wenye elimu kubwa. Yote hayo ni mazuri sana kwa hamasa na kutufundisha, lakini changamoto ni moja, yanakuonesha matokeo, alikuwa wapi na sasa yuko wapi. Hapo katikati ya alipokuwa na alipo sasa, pana muda wa siyo chini ya miaka 10 na kwa wastani ni miaka 30. Muda huo ni wa mchakato mgumu mno wa mtu kufika pale ambapo watu wanamshangilia sasa. Lakini watu hawapendi kuona hicho kipindi cha mchakato, wanapenda kuona matokeo, na hawapo tayari kuingia ule mchakato ambao watu wamepitia.

Tukienda kwenye biashara ndiyo kabisa dunia inamhadaa kila mtu. Kila siku utakutana na watu ambao wana fursa mpya, fursa ambayo kwenye hesabu za makaratasi ni kubwa mno. Ukielezwa unaweza kuacha kila kitu unafanya, ukamtukana hata mwajiri wako au kuacha kibiashara chako kidogo unachofanya na kuona umechelewa sana. Unaambiwa ukilima tunda fulani, mche mmoja unatoa matunda labda 100, kila tunda ni elfu moja, kwa hiyo mche mmoja unakupa siyo chini ya laki moja. Heka moja itaingia siyo chini ya miche 500, hivyo heka moja, ndani ya mwaka mmoja, itakupa siyo chini ya milioni 50. Hapo unakimbia na kuona umepitwa, lakini yapo mengi ambayo hujaambiwa au kuelezwa kwa wazi. Zipo changamoto ambazo hutaelezwa mwanzoni mpaka pale utakapoingia na kufanya.

Mambo mengi mno tumekuwa tunahadaiwa, ukikosa umakini rafiki yangu, utajikuta kila siku unakwama kwenye kila unalofanya. Hii ni kwa sababu taarifa nyingi unazopewa, siyo taarifa kamili. Zinaweza kuwa sahihi, lakini unapewa kwa upande mmoja, ule upande utakaokuhamasisha wewe uchukue hatua. Ule upande ambao unakufanya ufikiri kwa makini, huwa huelezwi.

Hivyo wajibu wako rafiki yangu ni huu, kuhakikisha unaupata ukweli wa jambo kabla hujaamua kuingia na kufanya. Taarifa unazopewa zipokee, lakini chimba ndani zaidi. Jielimishe kwa kujifunza na kusoma, halafu tafuta watu wawili waliofanya, mmoja aliyefanikiwa na mmoja aliyeshindwa. Kaa nao chini na jifunze, usiwaulize yale maswali ya kawaida, ambayo tayari wameshajikaririsha majibu kwa sababu wanaulizwa kila mara. Badala yake waulize maswali ambayo yatawafanya wao wenyewe kufikiri kwa kina.

Nimalize kwa kusema haya rafiki yangu , kuna tofauti kubwa sana ya kuwa na mtazamo hasi na kuwa makini. Watu wengi wamekuwa wanakimbilia kukubaliana na kitu kwa sababu wanaona wakikataa watakuwa na mtazamo hasi. Mimi ninachokuambia ni kama kitu hukielewi, kuwa na subira, huo siyo mtazamo hasi, bali ni kuwa makini. Mambo ya kufanya ni mengi mno katika hii dunia, kila kitu ni fursa. Ni muhimu sana uwe makini, uhakikishe chochote unachofanya unakielewa na unaendelea kukifuatilia kwa makini.

Usihadaike na dunia, na wala wingi wa watu usikufanye uache kufikiri kwa kuona hao wengi hawawezi kukosea, hakuna wanaokosea mara nyingi kama wengi. Hivyo mara zote unapojikuta upande wa wengi, kaa chini na tafakari kwa kina kama unaelewa kweli hicho unachofanya au umeingia tu kwa sababu ya wingi wa waliopo.

No comments