Update:

Waugua matumbo kwa kunywa maji machafu


Wananchi wa kata ya Mabogini wilayani Moshi katika mkoa wa Kilimanjaro wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya tumbo yakiwepo Typhoid na Amoeba mara kwa mara kurtokana na kutumia maji yasiyo safi na salama. Wakizungumza na Mwananchi mara baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa maji uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA), wananchi hao walisema wanalazimika kuamka usiku wa manane na kutembea umbali mrefu kutafuta maji. Mkazi wa kijiji cha mji Mpya, Rose Evarist, alisema katika eneo lao hawajawahi kupata maji safi na salama tangu miaka ya 1980 na badala yake wamekuwa wakitumia maji ya visima ambayo yamekuwa yakiwasababishia magonjwa ya tumbo. “Maisha yetu yamekuwa hatarini kwani tumekuwa tukiamka saa tisa usiku na kutembea umbali mrefu kuyafuata maji ambayo si safi na si salama kwa matumizi ya familia zetu,”alisema Evarist. Mkazi wa Mvuleni, Mariam Mwenda, alisema eneo hiyo ni kame hivyo inakuwa vigumu sana kupata maji kwa urahisi. Alisema wachuuzi wanawauzia ndoo moja ya maji ya lita ishirini kwa Sh500 na wengi wao wanategemea huduma ya maji kutoka kwenye mfereji wa umwagiliaji mashamba ya miwa ya kampuni ya TPC, ambayo nayo si maji safi na salama. Afisa mtendaji wa kata ya Mabogini, Masamba Charles, ameiomba serikali kupitia MUWSA kufanya utanuzi wa mtandao wa maji katika vitongoji vitatu vitatu vya Rau-Msufini, Sanya Line A na Mjohoroni. “Pia tunaiyomba serikali kuanzisha miradi ya Maji safi na salama ili kuhudumia vijiji vitano vya kata ya Mabogini vilivyosalia ambavyo vimekuwa na changamoto ya kupata majisafi na salama. Mkurugenzi mtendaji wa MUWSA, Joyce Msiru, alisema utekelezaji wa mradi huo umegharimu Sh317 millioni na mradi huo umetokana na mapato ya ndani ya mamlaka pamoja na wataalamu waliohusika.

No comments