Update:

Si ruhusa magari kusafiri lamu bila kusindikizwa na polisi
Mratibu wa masula ya usalama katika ukanda wa pwani nchini Kenya Nelson marwa ameonya kuwa magari yote ya umma na binafsi ambayo yanasafiri katika barabara ya Lamu-Mombasa bila ya kusindikizwa na polisi wenye silaha yatakamatwa na leseni zao kufutwa.

Marwa amesema sio ruhusa kusafiri katika barabara ya Lamu-Mombasa bila kusindikizwa na polisi,kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayotekelezwa na wanamgambo wa Al shabaab katika maeneo ya Lamu.

Akizungumza kisiwani Lamu wikendi iliyopita,mratibu wa masula ya usalama ukanda wa pwani Nelson Marwa alisema magari mengi yanayosafiri katika barabara ya lamu-mombasa yanakosa usalama wa polisi,ambao ni muhimu mno.

Marwa alisisitiza kuwa magari yote yanayosafiri Lamu ,hata yale ya shule na makanisa lazima yakaguliwe na polisi katika vituo vya doria barabarani,na kupewa askari kwa ajili ya kuwasindikiza.

"Tumesema magari yote yawe na usalama wa polisi.Kuna magari mengi ambayo yanasafiri bila kusindikizwa na polisi.Nilipokuwa nikisafiri kuja Lamu jana niliona magari mengi ambayo yanasafiri bila usalama wa polisi"

Wakati huo huo Marwa aliwaonya wasafiri kupanda magari ambayo yana polisi ndani,na kuepuka kupanda magari yasiyo na polisi.

Marwa aliwaonya madereva ambao wanahepa ukaguzi wa polisi kuwa ni hatia,na watachukuliwa hatua za kisheria.

"Maafisa wa polisi wamepanga ratiba ya kusindikiza magari.Wale ambao wansafiri bila usalama wa polisi wanahatarisha maisha yao"

Aidha Marwa alisisitiza kuwa kufuatia tamko la serikali,amri ya kutotoka nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi asubuhi bado itaendelea kutekelezwa,jambo ambalo halikupokewa vyema na wakazi na wafanyabisahara wa Lamu.

Wakazi wa Lamu wanalalamika kwamba amri ya kutotoka nje inawaathiri kiuchumi kwa sababu wengi wao ni wavuvi na wanategemea kwenda baharini nyakati za usiku kwa ajili ya uvuvi.

Amri hiyo ilitolewa wiki tatu zilizopita baada ya katibu wa kudumu katika wizara ya ujenzi Bi Maryam El Maawy kutekwa.

Bi Maawy pamoja na watu wengine sita walitekwa na wanamgambo wa Al shabaab,na baadae kuokolewa na wanajeshi wa Kenya.

Mratibu huyo wa masuala ya usalama eneo la Pwani Nelson Marwa ametoa agizo kwa maafisa wa usalama kuhakikisha kwamba watu wote wanaoingia na kutoka Lamu wanakaguliwa vilivyo kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari zao.

No comments