Update:

Waandishi walioripoti mkutano wa Lissu wahojiwa

Baadhi ya waandishi wa habari walioripoti mkutano wa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, uliofanyika Jumatatu ya wiki hii wamehojiwa na polisi. Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS) alifanya mkutano huo Jumatatu wiki hii ambapo pamoja na mambo mengine alilaani kukamatwa kwa wanachama wa Chadema. Leo, Ijumaa, Julai 21, Mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Ibrahim Yamola amehojiwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi ambao walifika katika ofisi za gazeti hilo. “Walitaka nifike Polisi Makao Makuu lakini tukakubaliana watakuja hapa ofisini kwetu asubuhi, wamekuja na wamenihoji kuhusu mkutano huo,” amesema. Yamola amesema watu hao walimuhoji mazingira ya mkutano huo, maneno aliyoyatamka Lissu na namna walivyoichapisha habari hiyo siku ya pili. Inaelezwa kuwa mwandishi mwingine wa gazeti la Mtanzania, Aziza Masoud naye anatarajia kuhojiwa baadaye leo.