Update:

Tanzania yapaa viwango vya soka vya FIFA


Timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepanda kwa nafasi 25 hadi nafasi 114 kutoka nafasi ya 139 kati ya mataifa 211 katika viwango vya ubora wa soka duniani vilivyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA jana.
Katika siku za hivi karibuni timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imekuwa ikicheza katika kiwango bora kabisa kilichoiwezesha timu hiyo kushinda katika michezo yake ikiwemo dhidi ya Burundi na Botswana katika mchezo wa kirafiki, Malawi pamoja na Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana katika michezo ya COSAFA inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Katika viwango hivyo vya mwezi Julai timu ya taifa ya Ujerumani inashika nafasi ya kwanza, Brazili ikishika nafasi ya pili, na timu ya Argentina ikishika nafasi ya tatu. Mataifa mengine ambayo timu zao zipo katika kumi bora ni pamoja na namba nne Ureno, Uswisi ikiwa ya tano, Poland ya sita. Chile ikachukua namba 7. Colombia ya nane, Ufaransa ya tisa na Ubelgiji ikishikilia namba 10.
Kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Uganda imeporomoka nafasi tatu mpaka kufikia 74, ikifuatiwa na Kenya kuanguka nafasi 10 mpaka 84, Burundi ikipanda nafasi 27 na kufikia 121, Rwanda imepanda nafasi moja na kufikia 127, Ethiopia ikidondoka kwa nafasi 11 na kufikia 136.