Update:

Rais Magufuli: ”Mnaotaka wenye Mimba Warudi Shule Muanzishe Shule Zenu”Rais John Magufuli amezitaka Asasi za Kiraia (NGO’s) kufungua shule kwa wanafunzi wanaopata mimba shuleni kama kweli zinawapenda wanafunzi hao.

Rais ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 4) alipokuwa akihutubia wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji Sengerema.

“Si kwamba nawachukia wenye mimba, hata kwa bahati mbaya akapata mimba, kama hizo NGO zinawatetea sana, zifungue shule za wenye mimba, kwa sababu zinawapenda wenye mimba, wafungue shule zao,”amesema Rais leo.

Amesema hata hao wanaofanya makongamano ya kuhamasisha watu wapate mimba wafungue shule zao kwa ajili ya wanafunzi hao.

“ Haiwezekani fedha za walipa kodi, Sh 17 bilioni kila mwaka za kusomesha watoto wetu, kwenda kusomesha wakinamama, wazunguke, waimbe, waseme nini mimi ndiyo Rais, huo ndio ukweli,”amesema.

Amesema tatizo si wanaopata mimba, kwani wapo waliopata matatizo, kama kuugua kwa muda mrefu wakashindwa kwenda shule lakini ulianzishwa mpango maalum wa kuwasomesha katika mfumo usio rasmi.