Update:

Pacha walioungana kufanyiwa kipimo cha MRI Muhimbili leo


Pacha walioungana leo wanafanyiwa kipimo kupitia mashine ya uchunguzi wa magonjwa ya MRI (Magnetic Resonance Imaging) ambayo itatoa majibu iwapo wana uwezekano wa kutenganishwa ama la. Watoto hao waliozaliwa katika Hospitali ya Misheni ya Berega iliyopo Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, Julai 21 mwaka huu jana walianza kuchukuliwa vipimo mbalimbali vya awali.  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aminiel Aligaesha amesema vipimo bado vinaendelea na watoto hao wapo chini ya uangalizi maalumu wa madaktari bingwa. “Jana walifanyiwa vipimo vya radiolojia kikiwemo cha CT–Scan na leo watafanyiwa kipimo cha MRI hiki sasa kitatujulisha kuhusu viungo vya ndani muhimu ikiwemo moyo, figo, ini na vinginevyo,” amesema Aligaesha. Amesema majibu ya kipimo hicho yatafanyiwa mashauriano na madaktari bingwa kwa kushirikiana kwa pamoja ili kuona ni namna gani watawasaidia pacha hao. “Suala hili linahitaji mashaurino ya wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwa kila mtu ana nafasi yake, tukishakamilisha tutatoa taarifa rasmi iwapo watoto hawa wameungana sehemu gani nini kitafanyika iwapo inawezekana kuwatenganisha au haiwezekani,” amesema Aligaesha. Amefafanua sababu ya MNH kuwaweka pacha hao chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kuwa ni kutokana na hali waliyonayo hivyo wamewaweka huko ili wasipatwe na madhara yoyote kiafya, “Tumewaweka humu ili kuwahudumia na kuwatunza kwa hali ya juu kuhakikisha wanapatiwa huduma zote kwa wakati.” Amesema.
source:mwnanchi

No comments