Update:

Mkurugenzi wa kompyuta wa IEBC akutwa amekufa


Mkurugenzi wa kitengo cha kompyuta (ICT) wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Chris Musando aliyepotea Ijumaa usiku amekutwa amefariki dunia. Polisi wamesema leo asubuhi kwamba mwili wa Musando pamoja na wa mwanamke ambaye bado hajatambuliwa imekutwa maeneo ya Kikuyu na imehifadhiwa katika chumba cha maiti. Mapema asubuhi gari lake aina Land Rover Discovery lilikutwa likiwa halijaaribiwa katika eneo la maegesho la TRM, barabara ya Thika saa 7.00 usiku wa kuamkia leo. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa jiji la Nairobi, Ireri Kamwende alisema gari hilo halikuaribiwa na msako umeimarishwa ili kumpata ofisa huyo mwandamizi. Mwenyekiti wa Tume, Wafula Chebukati alisema Musando alionekana kwa mara ya mwisho Ijumaa usiku. "Mawasiliano ya mwisho kutoka kwake yalikuwa ujumbe mfupi wa SMS ambao ulitumwa kwa mmoja wa marafiki zake saa 9.00 usiku wa kuamikia Jumamosi,” alisema Chebukati. Aliongeza kwamba ujumbe huo ulionyesha Msando alikuwa na fahamu zake na anayejua uelekeo wa siku hiyo. Musando alikuwa anajaza nafasi ya mkurugenzi wa ICT wa IEBC James Muhati ambaye alilazimishwa kwenda likizo ya siku 30 baada ya kushindwa kutoa ushirikiano na idara ya ukaguzi.

No comments