Update:

Mamba atishia amani Tanga


Wakazi wa Mitaa ya Kange na Mkurumuzi jijini Tanga wamesema maisha yao yapo hatarini kutokana na bwawa lilioibuka baada ya kubomoka bwawa la samaki la kiwanda cha Rhino kuwa na mamba wakubwa. Wakazi hao wamedai kuwa mwanamke mmoja alinusurika kuliwa na mamba mkubwa ambaye alikuwa amejificha katika kichaka. Licha ya kufikisha malalamiko yao katika mamlaka husika na kamati ya maafa ya Wilaya ya Tanga kutembelea, lakini ni miezi mitatu sasa hakuna hatua za kwuadhibiti wanyama hao zilizofanyika. Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Maopinduzi (CCM) Kata ya Maweni, Said Bindo (72) amesema hali ilivyo inavyohatarisha usalama wa wakazi wa mtaa huo na kuitaka Serikali kutosubiri maafa yatokee. “Tatizo hapa ni kwamba ni sababu huku wanaishi watu wa hali ya chini… kama wangekuwa wanaishi vigogo, hili bwawa lisingekuwepo. Kinachohitajika ni kutengeneza daraja litakalokuwa na uwezo wa kupitisha maji kwa wingi ili bwawa likauke,” amesema Kada huyo wa CCM. Bindo, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM tawi la Kange, amesema ameishi hapo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50 na haijawahi kutokea hali kama hiyo. “Sababu zinazotolewa tunaona kama ni visingizio… wanasema eti mara Halmsahuri itakapopata fungu, lakini kwa umri wangu na uzoefu nilionao, tatizo kama hili ni janga ambalo linahitaji kutatuliwa kwa fungu la dharura au kukiamuru kiwanda cha Rhino kujenga daraja kwa sababu ndiyo chanzo,” amesema Bindo. Issa Shaaban, ambaye nyumba anayoishi inapakana na mto huo alilalamika kuwa jana jioni mke wa kaka yake alikurupshwa na mamba mkubwa lakini alifanikiwa kukimbia na kujiokoa. Diwani wa kata ya Kange, Joseph Colyvirs, amesema tayari Baraza la Madiwani la Halmashauri ya jiji la Tanga limeshapitisha katika mpango wake wa kujenga makaravati katika mto huo ulioibuka hivi karibuni ili kuruhusu maji yapite. “Yupo mwekezaji alifanya kazi ya kuzibua pale lakini kutokana na maji kuwa mengi iimeshindikana,” amesema diwani huyo. Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa, amesema taarifa za kuibuka kwa bwawa katika eneo hilo anazo lakini tukio la kuonekana mamba halijamfikia na akaahidi kufanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha wananchi.

No comments