Update:

Fatma Karume: Lissu kanyimwa dhamana kwa amri toka juu

Wakili wa Tundu Lissu, Fatma Karume amesema polisi walikataa kumpa dhamana mteja wake jana jioni mara baada ya kukamatwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere. Akizungumza na Mwananchi, Karume alisema baada ya kufikishwa polisi, Lissu alitakiwa kuandika maelezo na kupewa onyo kwa kosa la uchochezi. “Lakini cha ajabu mpaka sasa hivi hatujaambiwa Lissu kamchochea nani, kosa la uchochezi lazima lilete madhara au uhalifu kwa wengine na ni lazima liwe la uhalifu.” Amesema Amesema hata walipouliza nani anayeweza kuruhusu mteja wake apate dhamana hiyo waliambiwa imezuiwa kwa amri kutoka juu. Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, (TLS) alikuwa akielekea Kigali, Rwanda, katika mkutano wa wanasheria wa Afrika. Karume amesema uchochezi lazima liwe ni jambo la uhalifu na mpaka sasa polisi hawajamwambia Lissu aina hiyo ya uchochezi. “Hili ni jambo la kisiasa, Lissu amezuiwa kwenda kwenye mkutano wa wanasheria wa Afrika, jambo hilo linawafanya hata wanasheria wote wa Afrika kujua mwenzao kakamatwa na Serikali,” amesema. Kwa mujibu wa Karume, Lissu amewapa ujumbe Watanzania akisema Aluta Continua, na kuwa yupo sawa