Update:

Watu 12 wauawa na kujeruhiwa kwa risasi Florida, MarekaniWatu 12 wameuawa na kujeruhiwa katika tukio la ufyatuaji risasi katika wilaya ya Orlando, jimboni Florida nchini Marekani.

Duru za kiusalama nchini humo zimeripoti kuwa, tukio hilo lilifanyika jana Jumatatu katika sehemu ya kazi, ambapo watu watano waliuawa na wengine saba kujeruhiwa.

Polisi katika eneo hilo wamesema tukio hilo halina uhusiano na ugaidi na yumkini limechochewa na ugomvi miongoni mwa wafanyakazi katika eneo hilo la viwandani karibu na barabara za Forsyth na Hanging Moss.

Mauaji haya yanafanyika wiki moja kabla ya maadhimisho ya mwaka mmoja, tangu watu wasiopungua 50 wauawe kwa kufyatuliwa risasi katika klabu moja katika mji wa Orlando, jimbo la Florida, moja ya matukio ya kutisha ya ufyatuaji risasi nchini Marekani katika miaka ya hivi karibuni.Kuongezeka matumizi ya silaha za moto nchini Marekani

Katikati ya mwezi uliopita wa Mei, matukio 61 yaliyotokea ndani ya masaa 24 na kupelekea watu wasiopungua 15 kuuawa na wengine 40 kujeruhiwa kwa risasi katika majimbo tofauti ya Marekani.

Kadhalika mapema mwezi huo, kituo cha takwimu za vitendo vya ukatili wa utumiaji silaha nchini Marekani kilitangaza kuwa watu 72 wameuliwa katika matukio ya ufyatuaji risasi yaliyotokea katika majimbo ya Texas, Kentucky na Carolina Kaskazini ndani ya masaa 48.

Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani (CDC), watu 33 elfu huuawa kila mwaka nchini humo, katika matukio ya ufyatuaji risasi.