Update:

Mghwira kuvaa kofia mbili

Wakati Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amekula kiapo Ikulu jijini hapa leo, Jumanne Chama cha ACT- Wazalendo kimesema kitajadili utekelezaji wa majukumu yake mapya na ya uenyekiti wa chama hicho. ACT imesema ilipokea taarifa ya uteuzi huo wakati Mghwira akiwa nje ya nchi hivyo baada ya kurejea, viongozi wa juu wa chama hicho pamoja na yeye walifanya mazungumzo kuhusu uteuzi huo. Mghwira aliteuliwa nafasi hiyo Juni 3, mwaka huu na Rais John Magufuli kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Saidi Meck Sadick aliyeamua kuachia ngazi ili vijana waendelee kufanya kazi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumanne na kuthibitishwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT, Ado Shaibu ni kuwa kufuatia uteuzi huo na uenyekiti na majukumu ya Mkuu wa Mkoa kamati ya uongozi wa chama itakutana kesho kwa ajili ya mazungumzo. Pamoja na mambo mengine chama kitajadili namna ambavyo Mghwira atatekeleza wajibu wake wa uenyekiti wa chama na majukumu yake mapya. “Chama kinatoa wito kwa wanachama wake kuendelea na utulivu wakati wa vikao vyake vya chama vinachukua hatua stahiki kuhusu jambo hilo,”imesema taarifa hiyo.