Update:

Wabunge wataka ma­MC, wapiga picha watozwe kodi

Kilio cha wabunge cha kutaka Serikali iongeze vyanzo vipya vya mapato, huenda kikapata jibu kesho kwenye Bajeti Kuu kama washereheshaji (ma­MC), wapiga picha na pango kutoka kwa wapangaji wa nyumba wataanza kutozwa kodi. Wakizungumza na Mwananchi jana, baadhi ya wabunge walisema Serikali inatakiwa kuongeza na kuimarisha vyanzo vilivyopo ambavyo havitumiki ipasavyo, hivyo kutochangia pato la Taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.

 Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Allan Kiula alisema kuna kila sababu ya kuimarisha sekta tofauti za uchumi kwa kuwa ndiyo tegemeo hivyo ikiyumba, makisio ya ukusanyaji kodi na mirabaha huwa hayafanikishwi. 

Alisisitiza haja ya watu wote kulipa kodi badala ya jukumu hilo kuachwa kwa wachache suala linaloweza kufanikishwa kwa kurasimisha maeneo yote yaliyosahaulika. 

Kiula alibainisha maeneo mapya ambayo yanaweza kuanzishiwa kodi kuwa ni ushauri elekezi, huduma za washereheshaji (ma­MC), wapiga picha pamoja na kuimarishwa kwa ukusanyaji wa kodi ya zuio ya asilimia 10 kutoka kwa wamiliki na wapangaji wa nyumba na makazi. “TRA wana uzoefu wa ukusanyaji na uhasibu wa mapato mbalimbali ya Serikali. Wakipewa ushirikiano kwenye sekta hii mchango wake utaonekana,” alieleza. Mbunge wa Nsimbo, 

Richard Mbogo alisema TRA inapaswa kuwekewa malengo makubwa ili watendaji wake wasugue vichwa kuyafanikisha na kupendekeza kodi kwenye mikataba ya kibiashara kati ya watu binafsi au kampuni. “Makadirio ya mapato lazima yawe juu wakati yale ya matumizi yakiwa chini. Makadirio ya bajeti lazima yawe juu siku zote kutokana na sababu mbalimbali,” alisema Mbogo.

 Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa aliishauri Serikali katika bajeti itakayosomwa bungeni kesho kuweka msingi wa maendeleo ya Taifa na kufanikisha ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati. Alisema ni muhimu kwa Serikali kuimarisha mfuko wa maji vijijini na tozo yake iongezeke kutoka Sh50 mpaka Sh100 kwa kila lita moja ya mafuta inayonunuliwa ili kufanikisha hilo.

 “Kwa sasa Sh128 bilioni zinakusanywa, lakini tozo ikiongezwa upo uhakika wa kupata kati ya Sh360 bilioni mpaka Sh400 bilioni zitakazofanikisha utekelezaji wa miradi husika,” alisema Ndassa. Mapendekezo ya mpango wa bajeti yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango yanaonyesha Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh31.6 trilioni kufanikisha matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kiwango ambacho ni ongezeko la Sh2.1 trilioni kutoka bajeti inayoisha ya Sh29.5 trilioni. 

Mwaka huo, Serikali inatarajia kutekeleza miradi ya kielelezo inayojumuisha uendelezaji wa mgodi wa makaa ya mawe Mchuchuma na Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam kupitia Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilomita 1,251 ambayo ni pana zaidi (standard gauge).

 Mingine ni uboreshaji wa Shirika la Ndege (ATC), ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi mkoani Lindi, uanzishwaji wa Kanda Maalumu za Kiuchumi mkoani Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma na uanzishwaji wa kituo cha biashara cha Kurasini pamoja na kusomesha vijana katika stadi za mafuta na gesi, uhandisi na huduma za afya.
Credit: Mwananchi

No comments