Update:

Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia kwenye familia – Waziri Mkuu


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wazazi wana jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu ili Taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia.Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

“Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na Taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema Waziri Majaliwa.

“Nitumie nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya Taifa tunalotaka kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisisitiza.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia sh. milioni 10 ambapo jumla ya sh. milioni 160 zilikusanywa. Kati ya hizo, sh. 111,150,000 zilikuwa ni ahadi, sh. 38,447,000 zilikuwa ni fedha taslimu na sh. 10,403,000 zilikuwa ni vifaa vya ujenzi.