Update:

Maalim Seif alaani adhabu ya Mdee, Bulaya

Siku chache baada ya Bunge kuwazuia wabunge Halima Mdee na Ester Bulaya kuingia vikao vyote vya Bunge hadi Bunge la Bajeti mwakani, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema vitendo hivyo ni mwendelezo wa kupigwa mateke kwa demokrasia Tanzania. Pia amesema hiyo ni ishara kuwa watawala waliopewa madaraka hawataki kufuata misingi ya demokrasia iliyopo. Mdee na Bulaya wote kutoka Chadema walikumbana na adhabu hiyo kutokana na vitendo vyao wakati Spika Job Ndugai alipoagiza Mbunge wa Kibamba, John Mnyika ambaye alipewa adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya Bunge hili linaloendelea, aondolewe ukumbini wakati wa mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini. Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, alionekana akimvuta shati mmoja wa askari waliokuwa wakimtoa Mnyika, wakati Bulaya wa Bunda Mjini alionekana akiwashawishi wabunge wa upinzani kutoka nje kuonyesha mshikamano kupinga uamuzi wa Spika. Maalim Seif alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na mwandishi wetu muda mfupi baada ya kushiriki hafla ya futari iliyoandaliwa na Baraza la Mtendeni Namba Mbili, lililopo Buguruni Mtaa wa Madenge, Dar es Salaam. Katibu mkuu huyo ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar katika Serikali iliyopita, alisema kitendo hicho si cha kiungwana na kinasikitisha kwa sababu wabunge hao ni wa majimbo ambao wanachaguliwa na wananchi. “Wananchi wa Kawe na Bunda wamewachagua hawa ili wakawasilishe kero zao. Sasa unawasimamisha muda mrefu wananchi wa maeneo haya si watakosa uwakilishi? Waingereza wanasema bila uwakilishi hatuwezi kutozwa kodi.Sasa leo wabunge wanazuiliwa, hivi wananchi wa Kawe na Bunda wakisema hawalipi kodi kwa sababu hawana mwakilishi mtawalaumu?” alihoji Maalim Seif. Alisema pamoja na maelezo mazuri ya kufuata kanuni, lakini watambue kuwa wanapo waadhibu wabunge, athairi ina kwenda kwa watu wengi ambao wanakosa mwakilishi katika chombo hicho kikuu cha kutunga sheria. Alisema CUF haikubaliani na jambo hilo na kudai kwamba hivi sasa kinachotumika ni wingi wa wabunge wa CCM ambao wanakanyaga misingi ya demokrasia. Msiba wa Ndesamburo Akizungumzia yaliyotokea katika mazishi ya mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, Maalim Seif alisema kitendo cha viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwanyima Chadema Uwanja wa Mashujaa ni mwendelezo wa kuwanyima haki wapinzani. Alisema baadhi ya viongozi wa Serikali na wabunge wa CCM walisikika wakitoa kauli za kumsifia Ndesamburo, kwamba alikuwa mzee mwenye hekima na mwenye kutoa michango mizuri alipokuwa bungeni. “Sasa ilipofika wakati wa kumsindikiza mwenzetu (Ndesamburo), wanaanza kuleta fujo. Tunaambiwa shughuli zote huwa zinafanyika Uwanja wa Mashujaa na Mahakama zinakuwapo lakini iweje kwa Ndesamburo haiwezekani,” alihoji Maalim Seif. “Kwa hili la Ndesamburo, hii inatoa picha kuwa hakutakuwa na shughuli za kijamii zitakazofanyika kwa sababu kuna Mahakama na vitu vingine,” alisema. Aliwataka viongozi wa Serikali kuacha tabia ya kuchagua mambo badala yake wawe na msimamo mmoja unaoeleweka, Maalim Seif alisema ni jambo la kawaida kwa wapinzani kuzuiwa kufanya baadhi ya mambo lakini ikitokea viongozi wa CCM wamefariki dunia watapitishwa mtaani. “Watu wa Moshi wamekosa fursa ya kumuaga mzee wao aliyekuwa mbunge kwa miaka 15. Yaani mnaweka vipingamizi hadi katika barabara ili watu wasitoe heshima ya mwisho? Narudia kusema tena hii ni alama kuwa demokrasia haina nafasi Tanzania,” alisema. Maalim Seif alitumia nafasi hiyo kumuomba Rais John Magufuli kutenda haki kwa watu wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa kwani yeye ni kiongozi wa Watanzania. “Wapinzani hawana tatizo na kuweka amani mbele ya Taifa hili. Mbona walivyoenda kumuaga Uwanja wa Majengo hakukuwa na vurugu zozote? Tusiogope watu, na viongozi lazima tuwaheshimu watu,” alisema. Katibu wa Baraza la Mtendeni Namba Mbili, Mohamed Ally Mwinyi alisema lengo la kuunda baraza hilo ni kuwakutanisha pamoja wanachama wa CUF na kujadali masuala ya maendeleo ya chama hicho. “Baada ya ofisi ya makao makuu kuchukuliwa na upande mwingine, tuliamua kuunda baraza kama hili ili kuimarisha chama. Tunakushukuru Maalim Seif kwa kujumuika na sisi kwenye futari,” alisema Mwinyi.
credit:Mwananchi;

No comments