Update:

Kipindupindu chaua mtoto, wengine 16 walazwa

Mtoto mwenye umri wa miaka mitano, amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu uliolipuka katika kijiji cha Samazi, wilayani Kalambo, Rukwa. Kadhalika watu wengine 16 wamelazwa kwenye zahanati ya kijiji hicho wakidaiwa kuugua ugonjwa huo. Akizungumza na gazeti hili ofisni kwake leo (Jumatano) Ofisa tarafa ya Kasanga, Peter Mankambila amesema kuwa chanzo cha ugonjwa huo ni wavuvi waliokuwa wametokea kijiji cha Mpasa kilichopo wilaya ya Nkasi, ambao walifika kijijini hapo kwa shughuli za uvuvi na kuwaambukiza wengine. Amesema ugonjwa huo uligundulika Juni 16, 2017 na mpaka sasa watu 16 wamelazwa kwenye zahanati ya kijiji hicho kwa matibabu zaidi. Kwa upande wake ofisa afya wa wilaya hiyo, Andondile Mwakilima ambaye licha ya kukiri kuwepo kwa ugonjwa huo, amesema hadi sasa watu wanane wameruhusiwa kurudi nyumbani na wengine wanane wakiendelea kutibiwa. “Tunaendelea kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kuchimba vyoo, kipindupindu kipo na kinaua,” amesema. Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Julieth Binyura amewasihi wakazi wa mwambao wa ziwa hilo kutumia maji safi na salama ili kujiepusha na ugonjwa huo.