Update:

DAWA YA KUTIBU MSONGO WA MAWAZO (STREES)

Moja ya vitu vinavyowasumbua watu kwenye zama hizi ni msongo wa mawazo au kama unavyojulikana kwa kiingereza STRESS. Tumefika hatua mpaka watu wanajisifia ni kwa namna gani maisha yao yana stress, kama vile ni kitu cha ufahari au ndiyo kuonekana una makubwa una pambana nayo.
Kwa namna yoyote ile, stress siyo nzuri, kiafya, kisaikolojia, kiakili na hata kimahusiano. Stress zinachochea magonjwa mengi kama vidonda vya tumbo, magonjwa ya moyo, magonjwa ya akili. Pia stress zinaathiri mahusiano mengi ya kifamilia na kijamii. 
Lakini hakuna popote utapata darasa la kuondokana na stress katika jamii zetu. Badala yake watu wanatafuta njia za mkato za kuondokana na stress zao, na wote huishia kwenye ulevi wa pombe au madawa ya kulevya. Njia hii hutoa suluhisho, ila ni la muda mfupi kwani ulevi ukishaondoka kichwani, uhalisia unarudi na stress zinakuwa pale pale. Kwa sababu hii, watu huongeza zaidi ulevi na mwishowe kujikuta wanategemea ulevi maisha yao yote. 
Kwa wale ambao stress zimepita kiwango na kwenda kwenye hali ya ugonjwa wa akili, wao hujikuta wanatumia madawa maisha yao yote. Dawa nazo hazina tofauti na ulevi, msaada wake ni kwa muda, na hivyo wasipotumia mambo yanarudi pale pale. Hili huwapelekea kuwa wategemezi wa dawa maisha yao yote.
Kwa hali hii ya mambo, tunaweza kujiuliza hivi kweli ipo dawa ya kuondokana na msongo wa mawazo, ambayo haina utegemezi? Na jibu ni ndiyo, na nitakushirikisha hapa njia hiyo.
Kabla hatujaijua dawa hii ya msongo wa mawazo, kwanza tuangalie ni kitu gani kinachozalisha msongo wa mawazo.
Stress inazalishwa pale mtu anapokuwa sehemu moja na mawazo yake yanamtaka kuwa sehemu nyingine. Upo hapo ulipo sasa, lakini mawazo yako yanataka uwe sehemu nyingine. Upo wakati wa sasa, lakini mawazo yako yapo wakati ujao. Hapa ndipo unapozalisha stress kwa sababu, hakuna lolote unaloweza kufanya kwa kule unakotaka kuwa, au kwa wakati ujao. Utajitesa kwa kufikiria vitu ambavyo huna pale ulipo sasa, na akili yako itasumbuka na msongo kuingia.
Kwa namna hii unatengeneza mpasuko ndani yako, huwi kamili popote ulipo, huwezi kufanya vizuri kile unachofanya hapo, na huwezi kubadili chochote kwenye kule unakofikiria. Mpasuko huu unakuwa mzigo kwako na unazalisha msongo wa mawazo.
Kwa kuelewa kinachozalisha stress, nafikiri wewe mwenyewe umedhajua dawa ya stress ni nini.
Ndiyo, rahisi kama hivyo; dawa ya stress ni kuwa pale ulipo, kimwili, kiroho na kiakili. Usiweke mwili sehemu moja na mawazo sehemu nyingine, utakuwa hujitendei haki na hutaweza kuchukua hatua yoyote kuboresha kile unachowaza.
Dawa ya uhakika ya stress, ambayo haina utegemezi ni kuwa pale ulipo kimwili, kiakili na kiroho. Usiruhusu mpasuko wowote ndani yako, kwa kuwa sehemu moja kimwili na sehemu nyingine kiakili.
Weka mawazo yako yote kwenye kile unachofanya kwa wakati husika, kipende na kukithamini na ona mchango mkubwa unaotoa kwa wengine kupitia kile unachofanya. kwa njia hii utakuwa na muungano ndani yako, ambapo mwili, akili na roho vyote vitaungana kufanya kitu chenye manufaa sana kwako na wanaokuzunguka. Na kadiri unachofanya kinavyokuwa bora, ndivyo wengi zaidi wananufaika na wewe kuridhika. Unaporidhika, huwezi kamwe kuwa na msongo wa mawazo.
Katika tafiti zote za kiafya, msongo wa mawazo siyo tatizo kwa watoto wadogo. Huwezi kumkuta mtoto mdogo, wa chini ya miaka saba anakuambia nina stress. Hii ni kwa sababu wao ulimwengu wao ni kile wanachofanya kwa wakati husika. Mtoto akiwa anacheza maisha yake yote yapo kwenye mchezo ule. Hachezi akifikiria baadaye atafanya nini, au kesho itakuwaje. Anaweka kila kitu kwenye mchezo ule na ndiyo maana wanafurahia.
Hata anapoadhibiwa, mtoto mdogo atalia kwa wakati ule alioadhibiwa, atakasirika, lakini muda huo ukishapita anaendelea na maisha mengine. Hutakuta mtoto mdogo akiwa na hasira na kununa kwa sababu jana aliadhibiwa.
Unaweza kusema hao ni watoto na hawajayajua maisha, lakini unachosahau ni kwamba, wanayoishi watoto ndiyo maisha. Japo simaanishi usijipe majukumu kama mtoto, badala yake uwe pale ulipo, ufanye kile unachofanya, ukishamaliza uende kwenye jambo jingine.
Na hii haimaanishi kwamba usahau kuhusu kesho, au usahau kuhusu yaliyopita.
Unachohitaji ni kukumbuka ulikotoka na kujifunza kwa yale uliyoshinda na uliyoshindwa pia, ili ujue hatua zipi za kuchukua na zipi za kuepuka. Pia uwe na maono makubwa ya siku zijazo, uwe na mipango mambo yapi unafanya na yapi hufanyi. Baada ya hapo, kuwa pale ulipo, fanya kile unachofanya.
Kila mwisho wako wa siku, pitia yale uliyofanya, na pia pangilia siku yako inayokuja. Panga mambo muhimu utakayofanya na yafanye, kama ulivyopangilia. Tenga muda wa dharura pia, na weka vipaumbele vikali kwenye maisha yako. Kama kitu hakipo kwenye kipaumbele chako, usikifanye, hata kama kila mtu anakifanya.
Zipo changamoto ambazo utakutana nazo kwenye maisha yakoya kila siku, ambazo zitakusukuma kufikiria zaidi wakati ujao, labda kwa kuona mambo yatakuwa magumu zaidi ya yalivyo sasa. Au kujikumbusha changamoto nyingine za nyuma, na kuona labda wewe ndiye una bahati mbaya tu. Hayo yote yanakuzalishia stress kwa sababu unakwepa changamoto iliyopo mbele yako na kufikiria wakati uliopita na wakati ujao. Dawa ni ile ile, kuwa pale ulipo, kaa na changamoto hiyo na uitatue, kwa hatua unazoweza kuchukua kwa hapo ulipo sasa. Na kama hakuna unachoweza kufanya, iweke pembeni na fanya kitu kingine, ambacho kitabeba mawazo yako yote.
Kwa namna yoyote ile, usiruhusu mawazo yako yawe sehemu ambapo mwili wako haupo kwa wakati huo. Usijiruhusu kufanya kitu kwa sababu tu unafanya, penda kila unachofanya, weka juhudi zaidi na mawazo yako yote yawe pale. Kwa njia hii hutaruhusu msongo wa mawazo kuingia kwenye maisha yako.
Msisitizo ni kuwa pale ulipo, ukifanya kile unachofanya, na kwa namna hiyo utafanya kwa ubora na kuwa na utulivu wa ndani yako. Hapo utasahau kabisa kitu kinaitwa msongo wa mawazo.

No comments