Update:

Chadema wataka Katiba Jaji ya Warioba irejeshwe
Chadema imesema iwapo Tanzania inataka kunufaika na rasilimali zake na kushinda vita vya kutetea utajiri wake inapaswa kwanza kurejesha katiba iliyopendekezwa na Jaji Joseph Warioba na si vinginevyo. Akitoa msimamo wa chama kutokana na kile kinachoendelea baada ya kutolewa kwa ripoti mbili za Rais kuhusu mchanga wa dhahabu, leo (Ijumaa) Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji amesema suluhisho la kudumu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa ni kurejea katika katiba ya wananchi. “Chadema tunasema kuwa haya yote tunayoyapigia kelele itakuwa ni kazi bure iwapo haturejeshi hoja ya katiba mpya. “Katiba ya Warioba iliweka mapendekezo ya jinsi ya kulinda rasilimali za taifa na kama tungefuata hayo yote hili la sasa halingepaswa kuwa na mjadala mkubwa kiasi hiki,” amesema wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni. Pia, chama hicho kimeitaka CCM kujipima na kujitafakari kama kinafaa kuendelea kuaminika kuongoza dola kutokana kushindwa kutetea vyema rasimali za taifa kwa kuruhusu mikataba mibovu.