Update:

Algeria: Utatuzi wa mgogoro wa Libya utatimia bila uingiliaji wa kigeniWaziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa, utatuzi wa matatizo ya Libya utatimia bila uingiliaji wa kigeni sambamba na kulindwa umoja wa kitaifa.

Abdelkader Messahel ameyasema hayo jana baada ya kikao cha pande tatu na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Tunisia kilichofanyika nchini Algeria na kuongeza kuwa, ushirikiano baina ya Misri, Algeria na Tunisia kwa upande mmoja na taasisi za kimataifa kwa upande wa pili kwa ajili ya kutatua matatizo ya Libya, ni wenye umuhimu mkubwa.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry amekaribisha juhudi endelevu za mazungumzo kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Kikao cha pande tatu cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni majirani na Libya, kimeanza nchini Algeria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry

Katika kikao hicho mawaziri hao wanajadili hali ya kisiasa na kiusalama inayotawala hivi sasa nchini Libya.

Hayo yanajiri katika hali ambayo kumeibuka mvutano mpya baina ya viongozi wa kisiasa nchini Libya kufuatia hatua ya Misri kufanya mashambulizi ya kijeshi kwa kushirikiana na kiongozi wa jeshi wa Libya. Kufuatia hali hiyo, wanaharakati nchini humo wametaka mkuu wa jeshi la nchi hiyo apandishwe kizimbani kwa madai ya kula njama na Misri na kutoheshimu haki ya kujitawala ya Libya.

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu alipoondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011 kufuatia uingiliaji wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.